Mtambo wa Umeme wa Shirika la Umeme (Tanesco) ulioko maeneo ya Ubungo jijini Dar es Salaam, jana ulilipuka na kusababisha maeneo kadhaa ya mji huo kukosa umeme kwa muda.
kwa habari zaidi...Akizungumza jana, Meneja Uhusiano wa Shirika hilo, Badra Masoud alisema ajali hiyo ilitokea jana majira ya saa moja asubuhi na ilisababishwa na matatizo ya kiufundi. Alisema line iliyolipuka ni ile ya kupokelea umeme kutoka mtambo wa Songas wa KV 132 ulioko katika maeneo ya shirika hilo, ambao hata hivyo ulizimwa kwa msaada wa Jeshi la Zimamoto na vifaa vya kuzimia umeme vya shirika hilo. Badra alisema Mkoa ulioathirika na kuungua kwa mtambo huo ni Dar es Salaam tu na kwamba mikoa mingine hali ni ya kawaida.
Alisema mafundi wanaendelea kufanya matengenezo na baada ya muda hali ya umeme itarejea katika hali yake ya kawaida katika maeneo yote ya Mkoa wa Dar es Salaam.
“Hakuna athari kubwa zilizotokea maana zimamoto walifika mapema na kuzima moto na vifaa vyetu vya zimamoto ambavyo viko kila kona vimesaidia sana, maana hapa kwasababu ya umeme tumeviweka maeneo mengi na vimetusaidia sana,” alisema Badra.
0 Comments