Chama cha Wamiliki wa Daladala Mkoa wa Dar es Salaam (Darcoboa), kimewaagiza wamiliki wa daladala kusitisha huduma Ijumaa wiki hii iwapo utaratibu wa kukamata daladala na kuzishikilia katika mazingira yasiyo ya halali, hautafutwa mara moja kabla ya siku hiyo.
Mwenyekiti wa Darcoboa, Sabri Mabruk, alisema jana kuwa hawana pingamizi na trafiki kukamata daladala, hawawezi kuuvumilia utaratibu huo kwa vile ni wa ukandamizaji.
Aksema trafiki wamekuwa wakikamata daladala na kuzipeleka kwenye ofisi za Wakala wa Umeme na Ufundi (Temesa), badala ya kituo cha polisi.
“Ukifika Temesa unamkuta trafiki anakuonyesha orodha ya namba za gari yako na kukwambia wiki iliyopita ulifanya kosa fulani kisha unapigwa faini kuanzia Sh. 200,000 kutegemea na kosa,” alisema Sabri.
Alisema hawajui nani anayepeleka namba za gari kwa trafiki, kwani wanapowauliza maofisa wa Temesa, hujibu hawajui.
Sabri alisema utaratibu huo ulianza taratibu na sasa umeota mizizi, umeleta athari kubwa, kwani daladala likikamatwa Ijumaa, linashikiliwa hadi Jumatatu, hivyo kuwakosesha mapato.
Alisema wamelazimika kuwasilisha kilio chao kwa vyombo vya habari baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini Nchini (Sumatra) kupiga kimya licha ya kuiandikia mara kadhaa barua za malalamiko.
Sabri alisema utaratibu huo wanaupinga kwa vile hauna kipimo cha kuthibitisha kosa na pia unapora uhuru wa mtuhumiwa kupelekwa mahakamani.
0 Comments