Timu ya taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ leo inashuka dimbani kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kuvaana na mabingwa watetezi, Uganda katika mechi yao kali ya nusu fainali ya kuwania ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la chalenji.
Mechi hiyo itaanza saa 11:00 jioni wakati baada ya kutanguliwa na nusu fainali nyingine itakayoanza saa 9:00 alasiri na kuzikutanisha Ethiopia na timu iliyoalikwa ya Ivory Coast, ambayo inaundwa na nyota wengi chipukizi.
Kocha wa Stars, Jan Poulsen, alisema kuwa kila mechi huwa na mipango yake ya ushindi na jana jioni alikuwa na kibarua cha ziada cha kuwapa wachezaji wake mbinu zaidi za kuwavua taji Uganda wanaosaka ubingwa wa michuano hiyo kwa mara ya tatu mfululizo.
Poulsen alisema kuwa timu yake imefanya mazoezi mbalimbali ya uwanjani na ili kujiandaa kupambana leo na hatimaye kusonga mbele, alitarajia kuongeza 'dozi' nyingine mpya jana, maalum kwa mechi ya nusu fainali.
"Siwezi kusema nini tutafanya, ila nitawaandaa ili watimize lengo letu la kushinda mechi hii," alisema Mdenmark Poulsen, aliyepata mafanikio makubwa katika mechi zake tatu zilizopita tangu aanze kuwaweka benchi washambuliaji wake nyota na kuwatumia zaidi viungo, akiwemo Nurdin Bakari aliyefunga magoli matatu katika mechi tatu alizoanza kutumikia jukumu jipya la upachikaji mabao.
Poulsen alisema kuwa hivi sasa anaridhishwa mno na jitihada za wachezaji wake uwanjani kwani wanajituma mno, jambo ambalo anaamini litaendelea hata katika mechi ya leo na hatimaye kutwaa ubingwa.
"Tulijituma ili tufurahi pamoja, tutaendelea na kasi hiyo. Tunajua nini cha kufanya, tunamuomba Mungu atusaidie na kutuongoza katika kufikia malengo yetu," nahodha wa Stars, Shadrack Nsajigwa, alisema wakati akizungumzia mechi yao dhidi ya Uganda.
Kipa chaguo la kwanza wa Stars, Juma Kaseja, alisema kuwa ushirikiano ndani na nje ya uwanja ndio utakawasaidia kushinda leo.
"Hakuna miujiza, tukiwa pamoja tutafanya vizuri, tumejiandaa vizuri na tunategemea kufanya vizuri, hayo ndiyo malengo ya kila mchezaji kikosini kwetu," aliongeza Kaseja.
Kocha wa Uganda, Mscotland Bobby Williamson, alisema kuwa leo anatarajia kutumia wachezaji wake wote wa kikosi cha kwanza ambao aliwakosa katika mechi iliyopita ya robo fainali dhidi ya Zanzibar kutokana na kuwa na kadi za njano.
Williamson alisema kuwa mechi ya leo inatarajiwa kuwa ngumu, lakini uzoefu wa wachezaji wake na kujituma ndio vitu anavyotarajia kumpa matokeo mazuri.
"Ni kazi sana kuwa bingwa mtetezi, timu zote zinataka kufanya vizuri na sisi ndio tunaangaliwa zaidi… naamini tutafanya vizuri ili tuweke rekodi," alisema kocha huyo ambaye ameiongoza timu hiyo kunyakua ubingwa wa Chalenji mara mbili mfululizo.
Stars walitinga nusu fainali baada ya kushinda 1-0 katika mechi yao ya robo fainali dhidi ya Rwanda juzi, huku Uganda wakishinda kwa mikwaju ya penati 5-3 dhidi ya Zanzibar.
Katika michuano ya mwaka jana nchini Kenya, Stars walilala 2-1 kwa Uganda na Machi mwaka huu, katika mechi yao ya kirafiki iliyochezwa kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, Uganda waliifunga Taifa Stars 3-2.
Timu zitakazoshinda katika mechi za leo zitakufana katika fainali itakayochezwa keshokutwa Jumapili huku zitakazifungwa zitacheza mechi ya utangulizi ya kusaka mshindi wa tatu.
0 Comments