Nyota ya kiungo wa timu ya taifa ya soka ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars na klabu ya Yanga ya jijini Dar es Salaam, Nurdin Bakari, imezidi kung'ara katika mashindano ya Kombe la Chalenji yanayoendelea jijini Dar es Salaam baada ya kocha wa timu ya ligi kuu Sudan ya El Hilal, Sredojevic Milovan 'Micho' kuyangaza nia ya kumsajili baada ya kuvutiwa na kiwango chake.
Akizungumza jana, Micho, kocha Mserbia aliyewahi kuifundisha Yanga, alisema kuwa amevutiwa na kiwango cha juu cha Nurdin na kuongeza kuwa sasa, atafanya mipango ya kumtwaa kutoka katika himaya ya Yanga.
Micho yuko nchini kusaka nyota wa kuwasajili katika klabu yake tajiri ya El Hilal na sifa zake kwa Nurdin, zimekuja siku chache tu baada ya kocha wa APR ya Rwanda, …… kusema vilevile kuwa amevutiwa mno kiungo huyo na kwamba atawasiliana na uongozi wa klabu yake ili waangalie uwezekano wa kumsajili.
"Amenivutia sana, anacheza vizuri na anajua kukaa katika nafasi kama mshambuliaji… sidhani kama atabaki Tanzania. Kama sikufanikiwa mimi, basi makocha wengine waliomuona watamsajili," alisema Micho.
Aliongeza kuwa ameanza kumfuatilia Nurdin kwa muda mrefu wakati akiwa na timu ya taifa, Taifa Stars na kusema kuwa, jambo jingine linalomvutia kwake ni namna anavyocheza kwa umakini na kujituma katika muda wote wa mechi.
Katika hatua nyingine, Micho alisema kuwa endapo Tanzania itawekeza katika misingi sahihi ya soka, itakuwa moja ya timu tishio katika kipindi cha miaka mitano ijayo na hiyo inatokana na juhudi za wachezaji wake ambazo zinaonekana katika mechi zao alizoshuhudia hivi karibuni.
Alisema kuwa wachezaji wengi wa Tanzania na Afrika, wana vipaji lakini tatizo lao ni kukosa misingi ya soka wanayotakiwa kuipata tangu wanapokuwa na umri mdogo.
Aliwataka pia waachane na ushabiki wa klabu ambao ukipewa nafasi, huharibu mafanikio ya timu za taifa.