JINA la Wabogojo si geni katika masikio ya wapenzi wa sanaa nchini Tanzania.
Ni msanii mwenye kipaji cha hali ya juu katika fani ya sarakasi, kutokana na uwezo wake mkubwa wa kujikunja mwili na kujibinua kiasi cha kupita hata kwenye tundu dogo ambalo binadamu wa kawaida hawezi kupita.
Kutokana na uwezo huo, Wabogojo ambaye jina lake halisi ni Athuman Ford amepachikwa majina mengi likiwamo la Spiderman. Hebu fuatilia mahojiano na msanii huyo ambaye hivi sasa anafanya fani yake hiyo nchini China.
Mwandishi: Nieleze historia yako.
Wabogojo: Familia yangu inatokea Singida, nilianza elimu ya msingi Buguruni Moto na nikiwa darasa la tatu nilihamia Dodoma na kumaliza elimu ya msingi katika shule ya Msingi Nkuhungu mwaka 1998.
Mwaka 1999 nilianza elimu ya sekondari katika shule ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima iliyokuwa Shule ya Mwenge na mwaka 2000 nikahamia Sekondari ya Ufundi ya Minja iliyoko Ugweno ambako nililazimika kurudia kidato cha kwanza.
Na hapo ndio ukawa mwisho wangu wa kuendelea na shule, baadaye nikaamua kwenda kusoma masomo ya ufundi rangi katika Chuo cha Veta Dodoma mwaka 2002.
Mwandishi: Ni mtoto wa ngapi katika familia yenu? Wabogojo: Mtoto wa kwanza katika familia ya marehemu Ford Athuman wa Kariakoo.
Mwandishi: Lini ulianza sarakasi na nini kilikuvutia kuingia fani hiyo na si nyingine?
Wabogojo: Nilianza sanaa wakati nikiwa mdogo sana. Bibi yangu mzaa mama alinisimulia na alikuwa akiniita mwanasesere hadi leo.
Sikuvutiwa na chochote katika fani hii ila sanaa ipo kwenye damu, sababu nilishajaribu kazi nyingi lakini sikubahatika. Mwandishi: Kati ya uimbaji na sarakasi ni fani ipi unaipenda zaidi?
Wabogojo: Uimbaji na sarakasi vyote navipenda lakini nipo kivitendo ama kiviungo zaidi.
Nina imani wengi wataelewa kipi nafanya. Mwandishi: Katika familia yenu kuna msanii yeyote? Kama ndio mtaje na anafanya sanaa ipi
Wabogojo: Katika familia yetu wapo wasanii Shamsa Ford ambaye ni mwigizaji na Razack Ford ambaye ni msanii lakini mpigapicha za video na pia ni fundi kompyuta.
Mwandishi: Kuna habari kuwa kabla ya kuondoka Tanzania ulitoa wimbo, unaitwaje na unaelezea kisa cha kweli?
Wabogojo: Wimbo nilioutoa kabla ya kuondoka unaitwa ‘Ukitaka ubaya dai chako’, ni kisa cha kweli kwangu na ninaamini kuna wengi kitakuwa kimewatokea.
Mwandishi: Katika wimbo huo kulikuwa na tafsiri ya viziwi, kwa nini ulifanya hivyo?
Wabogojo: Niliamua kuweka tafsiri ya viziwi sababu Serikali hata watu binafsi wanasahau sana watu wenye ulemavu. Sijawahi kusikia wimbo ambao una tafsiri ya viziwi labda upo lakini siujui.
Pia sanaa yangu huwa naonesha hata kwa viziwi, mfano mzuri mara nyingi nilikuwa nikiburudisha kwenye shule ya watu wenye ulemavu ya Sinza Maalumu, hii yote ni kutokana na kuamini kuwa sisi sote ni wamoja na tuna haki sawa.
Mwandishi: Elezea kiundani kazi unazozifanya?
Wabogojo: Kazi ninazofanya ni maigizo, vichekesho, kupaka rangi nyumba pia nimeshawahi kutembeza nguo, mayai, sambusa, maji kwa kifupi kokote mimi nipo inategemea na maisha yanavyokwenda!
Mwandishi: Je, unafanya mazoezi kila siku? Na ni mara ngapi kwa siku?
Wabogojo: Mazoezi huwa nafanya pale ninapopata muda.
Mwandishi: Je kuna maumivu yoyote unayosikia?
Wabogojo: Hapana, sisikii maumivu hata kidogo. Ila wakati mwingine ninaweza kukumbwa na tatizo hilo kama nimeacha kufanya mazoezi kwa muda.
Mwandishi: Je, kuna mahali umesomea sarakasi, kama ndio ni wapi na lini?
Wabogojo: Sarakasi sikusomea ila ni baadhi ya vikundi nilivyopitia ndio sanaa yangu ilizidi kukua kama Urafiki Sanaa Theatre mwalimu wangu alikuwa marehemu Hamis, Tengeza, Lizombe Kings Dodoma, Hiyari ya Moyo Dodoma na Dunia Inc Promotion ya Magomeni Kondoa, Dar es Salaam.
Mwandishi: Huko China umeajiriwa na kampuni gani na mkataba wako ni wa muda gani?
Wabogojo: Nimeajiriwa katika taasisi ya maonesho inayoitwa The House of Dancing Water. Ni vigumu kusema lini mkataba wangu utakwisha.
Mwandishi: Unalinganishaje fani ya sarakasi China na hapa nchini.
Wabogojo: Fani ya sarakasi China ni kazi ambayo inakubalika na kuna vyuo vya aina mbalimbali vya sanaa na si kama kwetu Tanzania ambako sanaa haitiliwi maanani.
Mwandishi: Sanaa imekusaidia nini wewe tangu uanze?
Wabogojo:Sanaa imenisaidia sana. Kwanza imenisaidia kukidhi mahitaji yangu ya kila siku na kusaidia wengine. Kwa kweli, sanaa hii ya sarakasi imenipa mafanikio mengi hata maisha yangu yamebadilika sasa. Namshukuru Mungu kwa kipaji alichonipa.
Mwandishi: Nani alikupeleka China?
Wabogojo: China nimekuja kutokana na kutafutiwa kazi, na kisha nikapata mkataba huu chini ya wakala wangu, Winston Rudlle, ambaye anamiliki kampuni ya Mother Africa Circus ya Tanzania na iliyoko Ulaya.
Mwandishi: Nini maana ya jina la Wabogojo?
Wabogojo: Kabla sijaeleza nini chanzo cha jina langu, ngoja nikueleze kuwa Wabogojo ni ‘Ukikichemsha sana kiazi au boga kisha ukijaribu kulishika linabogojoka’. Kutokana na hili watu wakaamua kuniita ‘Wakubogojoka’ na baadaye likabadilika kuwa Wabogojo.
Chimbuko la jina hili lilianzia nikiwa DDC Magomeni Kondoa nikiwa na kampuni ya Dunia Inc na hasa waliolianzisha walikuwa Hard Guy, Master Flash, Kabwe ambao walikuwa ni watangazaji katika kampuni ile.
Mwandishi: Nini kikwazo cha maendeleo katika sanaa yako Wabogojo: Vikwazo vipo vingi katika fani, kwa mfano nilipokuwa Tanzania kikwazo kikubwa ni malipo duni ingawa unakuwa unajulikana sana, lakini mfukoni hakuna kitu na ndiyo maana Kingwendu huwa anasema ‘umaarufu kunuka!”
Mwandishi: Kuna chakula chochote maalumu unachokula ili kulainisha viungo vyako?
Wabogojo: Kwa kawaida nakula chakula kiasi kila siku, lakini si nyama au vyakula vinavyokomaza mifupa na viunganishi.
Mwandishi: Kuna kitu kingine unachopenda zaidi ya sarakasi?
Wabogojo: Mbali na sarakasi, napenda kuogelea, kukutana na watu wa mataifa mbalimbali na kubadilishana nao mawazo.Pia napenda sana ucheshi. Mwandishi: Unaweza kuwashauri nini watu wanaotaka kuanza sanaa ya sarakasi au muziki?
Wabogojo: Kwa wanaotaka kuanza sanaa hii kwanza inatakiwa iwe katika damu yao au nisema kuwa wawe ni kitu wanachokipenda na si kama wanataka kupoteza muda, pili anatakiwa kuheshimu kazi yake na ya mwenzake na pia kuzingatia utaratibu wa mazoezi. Wajue kuwa mwanzo mgumu.
Mwandishi: Nini malengo yako ya baadaye kisanii na kimaisha kwa ujumla?
Wabogojo: Malengo yangu baadaye ni kuwa na kikundi cha sanaa za aina mbalimbali kama ilivyo sasa ambapo nina kikundi kiitwacho Wateule chenye makao yake makuu Dodoma Mjini ambacho nasadiana nacho kwa hali na mali katika sanaa ya ngoma na sarakasi.
Mwandishi: Katika maonesho unayofanya, umewahi kufanya sanaa yako mbele ya kiongozi yeyote maarufu?
Wabogojo: Nimekuwa nikionesha kazi yangu kwa viongozi maarufu wanaokuja huku (China) lakini kwa sasa siwezi kukumbuka majina yao.
Mwandishi: Ni tukio gani ambalo hutalisahau maishani mwako?
Wabogojo: Jambo ambalo kamwe sitaweza kusahau ni siku baba yangu mzazi (Ford) alipofariki dunia machoni pangu pale katika Hospitali ya Amana. Nilikuwa nimetoka Kanda ya Ziwa kutangaza kampuni fulani ya simu za mkononi na tukiwa huko, matatizo mengi tulipata, cha ajabu tuliporejea Dar es Salaam hatukulipwa fedha ya kazi tuliyoifanya na siku baba anafariki dunia nilipiga simu kuomba wanisaidie japo fedha ya vocha, lakini bosi akasema hana fedha na hali akijua kuwa kwa wakati huo nilikuwa ninakabiliwa na matatizo makubwa tu.
Mwandishi: Ni jambo gani lililowahi kukupa furaha zaidi maishani mwako?
Wabogojo: Jambo ambalo lilinipa furaha zaidi maishani mwangu ni pale wazazi wangu walipokubaliana na kazi yangu ya sanaa na kuniruhusu hata kama ni usiku wa manane kwenda kuonesha kipaji changu.
Mwandishi: Tueleze pia jambo lililowahi kukuhuzunisha zaidi tangu upate akili ya kujua mema na mabaya?
Wabogojo: Ni baada ya maisha ya baba kubadilika na ndugu, jamaa na marafiki kupotea ghafla wakati walikuwa wakipata msaada wa aina mbalimbali wakati wa raha lakini wakati wa shida wote hawakuonekana . Duh! Inauma sana na kupitia hili nimejifunza mengi.
0 Comments