Sakata la malipo ya fidia kwa Kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Dowans Tanzania Limited sasa ni kama sinema isiyoisha, kila uchao inaibua jipya huku ikiendelea kuigawa nchi.
Jana Mbunge wa Bariadi Mashariki (UDP), John Cheo, maarifu kama Bwana Mapesa, alimtaka Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, kwenda bungeni kuwaeleza wabunge na Watanzania, fedha za kuilipa Dowans Sh. bilioni 94 zinatoka wapi.
Cheo ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Fedha za Serikali (PAC) katika Bunge la Tisa, amesema kuwa Ngeleja anatakiwa kueleza kwa nini kuna uharaka wa kuilipa Dowans.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam sambamba na mkutano wa uwajibikaji uliohusisha wahisani na nchi za Afrika zinazopata misaada, Cheyo ambaye amekuwa kimpya kwa muda mrefu tangu kuanza kwa sakata hilo, alisema hajui na wala haoni hizo fedha zinazotaka kulipwa haraka haraka zinatoka wapi.
Mkutano huo pamoja na mambo mengine ulikuwa ukijadili kuhusu namna ya kuhakikisha nchi zinazopata misaada kutoka kwa wahisani zinaweza kuisimamia kwa ajili ya maendeleo na sio kufuata matakwa ya watu hao.
“Bado sijaona uharaka wa serikali kuilipa Dowans, lazima kama nchi tuangalie hasara tutakayoipata mara baada ya utekelezaji huo kufanyika,” alisema.
Aidha, alisema mchakato mzima wa ulipaji wa Dowans unaonyesha kwa jinsi gani nchi ilivyodhahifu katika mikataba.
“Tunapotengeneza mikataba lazima tuangalie hapo baadaye utatokaje, inasikitisha leo nchi tunagombana ili tuwe na uharaka wa kuilipa Dowans,” alisema na kuongeza:
“Waziri Ngeleja na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, wanatakiwa kuangalia wakati wakitekeleza hilo Watanzania ambao ndio walipa kodi je, hawataumia?” alihoji na kuongeza: Uharaka huo unadhihirisha wazi kuwa, bajeti tunazofanya hazina maana.”
NGELEJA ATAPATA WAPI FEDHA?
Alisema Waziri Ngeleja anatakiwa alieleze Bunge fedha hizo za malipo alizosema zitatoka wapi na kwa sasa zipo wapi.
“Ina maana serikali ina fedha ambazo imeziweka kibindoni kwa ajili ya kuilipa Dowans, kama ndio sioni maana ya karatasi za bajeti,” alisema Cheyo.
CHADEMA KUUNGA MKONO HOJA YA KAFULILA
Katika hatua nyingine Chadema wamesema watakuwa tayari kuiunga mkono hoja binafsi inayotarajiwa kuwasilishwa na Mbunge wa Jmbo la Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, kuhusu mgawo wa umeme na Dowans.
Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, aliyasema hayo mwishoni mwa wiki alipozungumza na na wandishi wa habari mjini Singida.
Alisema Watanzania hawakubali nchi iliyo maskini ilipe Sh. bilioni 94, kwa kampuni ambayo wamiliki wake hawajulikani, iliyoingia kwa njia zinazonuka rushwa kwa hiyo kuwalipa itakuwa ni kuzawadia ufisadi badala ya kuadhibu.
“Suala la Dowans lazima tukalizungumzie bungeni, nafahamu kwamba Mbunge wa Kigoma Kusini, Mheshimiwa David Kafulila, ametoa taarifa kwamba atapeleka hoja mahususi bungeni kuhusu Dowans,” alisema.
Kwa mujibu wa Lissu, yeye pamoja na wenzake siyo tu watamuunga mkono katika hoja hiyo, kwa sababu ina maslahi makubwa kwa wananchi wa walio wengi, bali pia watataka nyaraka zote zinazohusu Dowans na ilivyoingia, na wamiliki wake na mkataba wake vipelekwe bungeni kujadiliwa.
“Tutataka nyaraka zote zinazohusu hiyo kesi ya Dowans dhidi ya Tanesco na serikali ya Tanzania ziletwe bungeni ili wabunge wajiridhishe kwamba kilichofanyika ni kisafi, tufahamu wenye Dowans ni akina nani, mawakala wao Tanzania ni kina nani,” alisema Lissu na kuhoji:
“Ofisi zao ziko wapi, huo mkataba walioingia na Richmond na baadaye Tanesco una uhalali gani, kesi walioipeleka dhidi ya Tanesco serikali ya Tanzania ilikuwa inadai nini, majibu ya utetezi wa Tanesco na serikali yalisemaje, majibu yaliyotolewa mpaka tukashindwa kesi yakoje?”
Lissu alionya kuwa ikiwa Bunge litaridhika kwamba kilichotokea ni ufisadi, watalazimika kuchukua hatua za kuwaeleza Watanzania wasikubali malipo kwa Dowans.
“Kwa sababu kama ambavyo tumezungumza siku nyingi sisi viongozi wa Chadema na chama chetu hatuko tayari kunyamazia ufisadi katika nchi hili kwa hiyo Dowans hatutainyamazia,” alisema.
DK. MVUNGI: HAIWEZEKANI KULIPANA NJE YA MAHAKAMA
Mhadhiri Mwandamizi wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Sengondo Mvungi, amesema hukumu ya Dowans dhidi ya Tanesco iliyotolewa na ICC haiwezi kusajiliwa nje ya mahakama.
Dk. Mvungi alisema hukumu hiyo haiwezi kusajiliwa nje ya mahakama kwa vile mahakama ndicho chombo kinachoweza kuruhusu hukumu yoyote ya upatanishi kutekelezwa kama hukumu ya mahakama.
Kuhusu hukumu hiyo kwamba, inaweza kusajiliwa kwa mwanachama wa ICC popote duniani, Dk. Mvungi alisema madai hayo hayana ukweli kwa vile mahakama hiyo haiundwi na dola, bali huundwa na pande zinazodaiana.
Alisema pia ni fikra potofu kudhani kwamba, Dowans wanaweza kukamata mali za Jamhuri ya Muungano zilizo nje ya nchi iwapo hawatalipwa fidia ya Sh. bilioni 94, ambazo Tanesco imeamriwa na ICC kuwalipa.
“Jamhuri haina mali zinazokamatika nje ya nchi. Mali yetu iliyo nje ya nchi ni majengo na samani zake za ubalozi tuliyonunua. Hata hivyo, nayo yamelindwa na sheria za kimataifa. Pia Jamhuri si mhusika katika kesi ya Dowans kwa sababu haina mkataba na Dowans. Sasa watakamata mali gani za Jamhuri na kwa sababu gani?
“Kwa hiyo, tunabishana na matapeli, ambao wako hata serikalini,” alisema Dk. Mvungi alipozungumza na NIPASHE jana.
NAPE SIAMINI YA KAMATI KUU
Naye Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Nape Nnauye, amesema haamini kamwe, kama taarifa iliyotolewa na Kamati Kuu ya Chama hicho iliyodai kwamba lazima Dowans ilipwe, ni yakweli.
Aidha Nape alisema haamini masikio yake kwamba kamati Kuu ya CCM anayoifahamu, inaweza kutoa taarifa mbaya kama hiyo.
Mwanasiasa huyo aliyasema hayo alipozungumza na gazeti hili kwa njia ya simu, baada ya kuombwa atoe maoni yake kuhusu maamuzi ya Kamati Kuu.
“Siamini kwamba yale niliyoyasikia juu ya kuwalipa Dowans ni uamuzi wa Kamati Kuu ya CCM ninayoifahamu,” alisema Nape.
Akifafanua alisema kinachomfanya asiamini kwamba uamuzi huo umefanywa na Kamati Kuu ya CCM, ni mazingira yaliyotumika kufikia maamuzi hayo.
Aliyataja mazingira hayo kuwa ni Kamati Kuu kuwa na mweleko wa wazi wa ‘kushabikia’ hukumu iliyotolewa na ICC, bila hata hukumu hiyo haijasajiliwa nchini.
Aidha, alitaja utata mwingine kuwa ni hatua ya Kamati Kuu kutoa maamuzi hayo ya kuibeba Dowans, huku ikijua wazi kwamba kuna utata mkubwa juu ya wamiliki wa Richmond, iliyorithisha mikoba yake kwa kampuni hiyo.
Vilevile alisema katika mazingira ambayo kuna asasi za kiraia ambazo zimefungua kesi mahakamani kupinga malipo hayo, haamini kwamba Kamati Kuu inaweza kutamka kwamba malipo ya Dowans hayaepukiki kwa kuwa ni mambo ya kisheria.
“Chama changu (CCM) ninachokifahamu sana si rahisi kutoa maamuzi kama hayo,”alisema Nape.
Alisema ana mashaka makubwa kama kweli taarifa iliyotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM John Chiligati, ndiyo hasa ilibeba maamuzi ya Kamati Kuu ya Chama hicho.
“ Nina mashaka kama ripoti iliyotolewa ndiyo yalikuwa maamuzi ya Kamati Kuu ya Chama changu,” alisema.
Alipoulizwa iwapo atathibitishiwa kwamba ni kweli taarifa ya Chiligati ilibeba maamuzi ya Kamati Kuu, Nape alisema atatoa maamuzi yake wakati huo.
0 Comments