Mwape aliyejiunga na Yanga katika kipindi kilichopita cha usajili maarufu kama 'dirisha dogo' akitokea katika klabu ya Kankola ya Zambia, alianza kampeni yake ya kuwania kiatu cha dhahabu cha ufungaji bora kwa kuifungia timu yake goli la kuongoza katika dakika ya 44 na akawahakikishia ushindi wana Jangwani kwa goli la pili dakika 10 kabla ya mechi kumalizika.
Kwa ushindi huo, Yanga, timu pekee ambayo haijapoteza mechi hadi sasa msimu huu, imeendelea kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi kwa kufikisha pointi 31, nne zaidi ya Simba walio katika nafasi ya pili kwa pointi 27. Hata hivyo, Simba, ambao juzi walikumbana na kipigo chao cha tatu msimu huu kwa kulala 3-2 mikononi mwa Azam, wana mechi moja mkononi.
Yanga waliozungukwa na migogoro ya kiongozi klabuni, walionekana kupuuza yanayotokea Jangwani kwa kuanza mechi ya jana kwa kasi ambapo katika dakika ya kwanza tu kipa wa Polisi, Salum Kondo alilazimika kufanya kazi ya ziada kuokoa shuti la kiungo Godfrey Bonny aliyewachambua mabeki wa timu hiyo ya 'maafande' kabla ya kufumu shuti hilo.
Mwape, ambaye Ijumaa alifunga magoli matatu katika ushindi wa 6-1 dhidi ya AFC ya Arusha, alipiga shuti zuri tena katika dakika ya 15 lakini kipa Kondo alilidaka kiufundi na Polisi, ambao walikuwa wa kwanza kuwafunga Simba msimu huu, wakajibu shambulizi hilo dakika sita kupitia kwa Pascal Maige, ambaye hata hivyo alishindwa kulenga lango kufuatia kujichanganya kwa walinzi wa Yanga, Nadir Haroub 'Cannavaro' na Iscak Boakye.
Semsue Juma alianguka mwenyewe ndani ya 18 ya Yanga katika dakika ya 30 na kushindwa kuiwahi pasi safi ya Seif Mohammed na kupoteza nafasi ya kufunga.
Mzambia Mwape alifunga goli la kwanza baada ya kumzidi ujanja beki wa Polisi, Noel Masakwa na kufumua shuti lililomshinda kipa na kufanya matokeo yawe 1-0 hadi mapumziko.
Nsa Job aliyeingia kutokea benchi katika dakika ya 53 kuchukua nafasi ya Idd Mbaga, alipoteza nafasi ya kufunga dakika mbili tangu aingie uwanjani baada ya kufumua shuti nje ya lango akiwa amebaki yeye na kipa Kondo.
Yanga waliendelea kupoteza nafasi za magoli wakati mshambuliaji Jerry Tegete aliposhindwa kufunga katika dakika ya 70 kufuatia kupiga 'kishuti-mtoto' kilichoishia mikononi mwa kipa wa Polisi.
Mwape alifunga goli lake la tano katika mechi mbili, kufuatia pasi ya Tegete kabla ya kumzunguka beki wa Polisi, Nahoda Haji, kabla ya kufumua shuti lilienda moja kwa moja wavuni.
Mwape sasa anashika nafasi ya tatu kwenye orodha ya wafungaji wanaoongoza akiwa na mabao matano sawa na mshambuliaji wa Simba, Mussa Hassan 'Mgosi'. Kinara wa mabao, Gaudence Mwaikimba wa Kagera Sugar ana magoli saba akifuatiwa na Jerry Tegete wa Yanga mwenye magoli sita.
Vikosi vilikuwa; Yanga: Yaw Berko, Shadrak Nsajigwa, Stephano Mwasika, Nadir Haroub, Isaack Boakye, Godfey Bonny, Nurdin Bakari, Omega Seme, Idd Mbaga/ Nsa Job, Davies Mwape, Jerry Tegete.
Polisi: Salum Kondo, Nahoda Haji, Elias Maftah, Noel Masakwa, Salmin Nkulo, Paschal Maige, Khalid Ali, Seif Mohamed, Semsue Juma/ Mohamed Neto, Delta Thomas.
Wakati huo huo, Yanga jana imemtangaza nyota wao wa zamani Salvatory Edward kuwa meneja mpya, uteuzi ambao ulifuatia barua ya kujiuzulu iliyowasilishwa jana na aliyekuwa meneja, Emmanuel Mpangala.
0 Comments