MLINZI aliyeshitakiwa kwa kuvunja na kuiba katika kiwanda cha Tanzania Distilleries Limited (Konyagi), Samwel Elias (24) amedai kuwa, aliiba katika kampuni hiyo lakini hakuvunja.

Mshitakiwa huyo, ambaye alikuwa mlinzi wa kampuni ya KK Securities ametoa madai hayo leo katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam wakati alipokuwa akijibu mashitaka ya awali yaliyosomwa na Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Basil Pandisha.

Mbele ya Hakimu Mfawidhi Kassim Mkwawa, Elias amekana kosa la kuvunja na amedai kuwa aliingia ndani ya stoo hiyo baada ya kupewa funguo na mtunza funguo wa ghala la kampuni hiyo, Beatrice Mushi.
"Nakubali kuiba mifuko katika kiwanda cha Konyagi, lakini hatukuvunja ila tuliingia ndani ya ghala baada kupewa funguo na mtunza stoo Beatrice ambaye alituagiza tutoe mzigo huo," amedai Elias.

Akijibu swali aliloulizwa na Hakimu Mkwawa kuwa ni nani alishirikiana naye kuutoa mzigo huo, mshitakiwa huyo aliwataja washitakiwa Said Mussa na Abraham Peter.

Alipotakiwa kueleza washitakiwa hao waliingizwaje katika kesi hiyo, alidai kuwa wao walifika katika kiwanda hicho kwa ajili ya kuchukua mzigo kama walivyoagizwa na Beatrice.

Washitakiwa hao wanadaiwa kuwa Novemba 15 mwaka jana saa 8 usiku, katika barabara ya Mbozi jijini Dar es Salaam, walivunja kiwanda cha Konyagi na kuiba katoni 44 za mifuko ya kuhifadhia kinywaji aina ya Konyagi viroba yenye thamani ya Sh. milioni 7.5 mali ya Tanzania Distilleries Limited.

Kesi hiyo itasikilizwa tena Februari 14 mwaka huu, washitakiwa wote wapo nje kwa dhamana.