Polisi mjiini Cairo wametumia gesi ya kutoa machozi na mabomba ya maji kujaribu kuzima maandamano yasio ya kawaida ya kuipinga serikali nchini Misri.Maelfu walijiunga na maandamano hayo baada ya kampeni zilizoendeshwa kupitia tovuti ambayo ilihamasishwa na harakati za nchini Tunisia.
Waliandamana katika mitaa ya Cairo na maeneo mengine wakipiga makelele ya kuipinga serikali, baada ya wanaharakati kuitisha siku ya mapambano katika ujumbe uliowekwa katika tovuti.
Si kawaida kufanyika maandamano ya kuipinga serikali nchini Misri ambako Rais Hosni Mubarak amekua akitawala tangu mwaka 1981 bila kuvumilia upinzani .
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton, alisema serikali yake inaunga mkono haki za kimsingi za watu kukusanyika na kutoa maoni yao na kuhimiza pande zote kuonyesha uvumilivu.
Aliongeza kwamba Marekani inaamini serikali ya Misri ni tulivu na inatafuta njia za kutimiza matakwa halali ya wananchi wa Misri. .
Matukio haya ya mjini Cairo yalipangwa katika kurasa za Facebook - maelfu ya waandamanaji walijiunga na kurasa hizo wakisema wangeshiriki.
0 Comments