Serikali imeifunga Zahanati ya CHO ya Ukonga Mazizini, jijini Dar es Salaam, baada ya kifo cha mzazi Sabela Mganga(31), aliyejifungua mapacha, na kuzuiliwa kwenda kupata tiba zaidi katika hospitali ya Amana hadi alipe deni.
Baada ya kujifungua kwenye zahanati hiyo, Daktari aliyekuwa zamu, Dk. Babu Machondela, alishauri
mzazi huyo ahamishiwe hospitali ya Amana kwa ajili ya kuongezewa damu, lakini wauguzi walikataa.Licha ya ushauri huo wa daktari, wauguzi walimshilikia wakidai kuwa hawezi kuondoka hadi atakapolipa deni la shilingi 155,800 anazodaiwa na zahanati hiyo kwa huduma ya kujifungua.
Hali ya mzazi huyo iliendelea kuwa mbaya hadi alipofia kwenye zahanati hiyo.
Baada ya kupata taarifa hizo, halmashauri ya Manispaa ya Ilala, iliunda timu maalum kuchunguza chanzo cha kifo mzazi huyo.
Akizungumza jana, Mganga Mkuu Manispaa hiyo, Asha Mahita, alisema ripoti ya uchunguzi wa tukio hilo umekamilika na anayeweza kuitoa kwa umma ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala.
Mahita alisema zahanati hiyo imeshafungwa na hatua zingine zitafuata baadae.
Isabela alipelekwa katika zahanati hiyo tangu Februari 5 hadi 7 na kujifungua watoto mapacha, lakini baada ya kujifungua hali yake ilizidi kuwa mbaya kutokana na kuishiwa damu.
Dk. Babu Machondeka alitoa maelekezo kwamba apelekwe Hospitali ya Amana kwa ajili ya matibabu zaidi ikiwa ni pamoja na kuongezewa damu.
Alipozungumza mara baada ya kifo hicho, kaka wa marehemu Christopha Chakulanga, alisema kuwa marehemu alipelekwa katika Zahanati hiyo ambayo ni ya mtu binafsi kwa ajili ya kujifungua.
Alisema alipofikishwa katika zahanati hiyo Februari 5 mwaka huu alijifungua mapacha wawili na baada ya hapo hali yake haikuwa nzuri kwani alipungukiwa na damu kwa kiwango kikubwa.
Chakulanga alisema baada ya kuona hali yake inaendelea kuwa mbaya, waliiomba zahanati hiyo kumruhusu kwa ajili ya kupelekwa katika Hospitali ya Amana kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi.
Alisema kiasi cha fedha walichotakiwa kulipa ni shilingi 60,000 kwa ajili ya huduma ya kujifungua ila zahanati hiyo iliwataka kulipia Sh. 155,800.
Alisema hawakuwa na kiasi hicho na walikuwa na 30,000.
Chakulanga alisema hali ya marehemu ilizidi kubadilika na kuwa mbaya zaidi lakini walipomuomba muuguzi aliyekuwa zamu kumruhusu ili wampeleke katika Hospitali ya Amana kwa ajili matibabu alikataa.
“Kwa kweli walivyonikatalia nisiondoke na mgonjwa wangu niligombana nao kwani hali ya mgonjwa ilizidi kuwa mbaya halafu muuguzi akawa mkali eti akituruhusu atakatwa fedha hizo katika mshahara wake,” alisema Chakulanga
Aidha, alisema walipoufikisha mwili wa marehemu Hospitali ya Amana walitakiwa kuonyesha kumbukumbu za alikotokea mgonjwa huyo ili kutambua kifo hicho kilitokana na nini.
Alisema walirudi katika zahanati hiyo ila hawakuweza kupata taarifa yoyote juu ya matibabu ya mgonjwa huyo ili waipelekea katika hospitali ya Amana.
Chakulanga alisema Hospitali ya Amana iliwapatia taarifa kuwa marehemu huyo alifariki kutokana na ukosefu wa damu katika mwili wake.
0 Comments