Wanaume 316,417 mkoani Tabora wanatarajiwa kufanyiwa tohara, ikiwa ni jitihada za serikali zinazoendelea za kupunguza kasi ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi nchini.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk Leslie Mhina, amewaeleza waandishi wa habari kwamba, kazi hiyo imeanza juzi na operesheni hiyo itaendeshwa katika hospitali zote za wilaya pamoja na vituo vya afya.

Amesema, kulingana na mwongozo uliotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa kuzingatia utafiti ulizofanywa sehemu mbali mbali duniani, imebainika kuwa tohara kwa wanaume inasaidia kupunguza kasi ya maambukizi ya VVU kwa asilimia 60.

Kwa mujibu wa Mhina, ili kuepukana na matatizo ya kuambukizwa ugonjwa wa Ukimwi kwa urahisi pamoja na kuambukizwa magonjwa ya zinaa, wanaume ambao hawajapata tohara wanapaswa kujitokeza wafanyiwe.

Amesema, shughuli hiyo itawahusisha wanaume kuanzia miaka 10 hadi watu wazima.

Amewataka wazazi wenye watoto walio katika kundi hilo, kuwapeleka wakafanyiwe tohara.

Dk. Mhina alitaja wilaya na idadi ya wanaume ambao hawajafanyiwa tohara na idadi yao kwenye mabano kuwa ni Tabora ( 56,066), Uyui (45,025), Nzega (72,407), Urambo (64,136), Igunga (56,410) na Sikonge ni wanaume 23,373.