Rais Jakaya Kikwete, na viongozi wenzake wa Afrika wanaotafuta ufumbuzi wa mzozo wa kisiasa nchini Ivory Coast, juzi walikutana kwa zaidi ya saa tatu na mmoja wa viongozi wawili waliojitangaza marais wa nchi hiyo.(Pichani viongozi hao wa nchi zilizokubaliana kuleta suluhu zikijadiliana kabla ya kikao chao cha pamoja)
Taarifa ya Ikulu jana ilisema Rais Kikwete na viongozi wenzake wa nchi kutoka Mauritania, Chad na Afrika Kusini, walikutana na kufanya mazungumzo na Laurent Gbagbo, mmoja wa wanasiasa ambao wamejitangaza kuwa Rais wa Ivory Coast kufuatia uchaguzi mkuu wa Novemba 18, mwaka jana.

Kwa muda mwingi wa mkutano huo katika Ikulu ya Ivory Coast mjini Abidjan, viongozi hao walimsikiliza Gbagbo na kumuuliza maswali katika hatua hiyo ya kwanza ya kazi ya ujumbe wa viongozi hao ambao ni kuwasililiza na kuwauliza maswali wadau wote katika(Pichani raisi Kikwete kushoto,raisi wa Maurirania,na Mpinzani mkubwa wa Gbagbo bwana Ouattara anayesemekana alishinda uchaguzi,na raisi wa South Africa Bwana Jacob Zuma).
mzozo huo ambao umeiacha Ivory Coast ikiwa na marais wawili, Serikali mbili na uwezekano mkubwa kuwapo makundi mawili ya watu wenye silaha na waliko tayari kuzitumia kuwania madaraka ya kuongoza nchi hiyo.
Katika mkutano huo, Gbagbo aliwahakikishia viongozi hao kuwa yeye ndiye Rais halali wa Ivory Coast kwa sababu alishinda raundi ya pili ya upigaji kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana nchini humo.
Viongozi hao wako Ivory Coast kutekeleza azimio la Umoja wa Afrika (AU) ambao katika Mkutano wa Wakuu wa nchi za AU mwezi uliopita mjini Addis Ababa, Ethiopia, uliteua kundi la nchi sita za Afrika chini ya uenyekiti wa nchi ya Mauritania kutafuta suluhisho la amani katika Ivory Coast.
Nchi zinazounda kundi hilo chini ya uenyekiti wa Mauritania ni Tanzania, Afrika Kusini, Chad, Burkina Faso, Equatorial Guinea ambayo ndiyo Mwenyekiti wa sasa wa AU pamoja na Nigeria ambayo ndiyo Mwenyekiti wa Jumuiya ya Uchumi ya Afrika Magharibi (Ecowas).
Nchi hizo zilifanya kikao cha kwanza Jumapili ya wiki iliyopita mjini Nouakchott, Mauritania kabla ya kusafiri kuja mjini Abidjan kukutana na pande zote zinazovutana katika mzozo huo wa kisiasa wa nchi hiyo ya Ivory Coast.
Kutwa nzima ya jana, viongozi hao walipanga kukutana na makundi ya watu na taasisi mbalimbali za wadau wa suala hilo la Ivory Coast.
Miongoni mwa waliotarajiwa kukutana na marais hao jana ni pamoja na Alassane Quattara, ambaye kama alivyo Gbagbo, amejitangaza kuwa Rais wa Ivory Coast kufuatia matokeo ya uchaguzi mkuu huo wa mwaka jana na pia naye ameunda serikali yake.
Makundi mengine yanayokutana na viongozi hao leo ni Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa katika Ivory Coast, Choi; wajumbe wa Baraza la Katiba la Ivory Coast, wajumbe wa Jeshi la Ivory Coast, wajumbe wa Tume ya Uchaguzi ya Ivory Coast kwa upande wa Gbagbo, Mkurugenzi wa Sekretarieti ya Serikali ya Quattara na wajumbe wa Tume ya Uchaguzi ya Ivory Coast kwa upande wa Quattara.
Mikutano mingi inafanyika kwenye Hoteli ya Pullman ambako wamefikia viongozi hao wa Afrika, isipokuwa ile mikutano inayomhusu Quattara itakayofanyika kwenye Hoteli ya Golf, mjini Abidjan, ambako kiongozi huyo amejichimbia pamoja na serikali yake.
Katika raundi ya pili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo ilimtangaza Quattara kuwa mshindi.
Lakini Baraza la Katiba ya nchi hiyo lilibadilisha matokeo kwa kutangaza Gbagbo kuwa mshindi baada ya kufuta matokeo ya kura katika majimbo saba ya wilaya 13 za eneo la kaskazini mwa nchi hiyo ambako ndiyo ngome ya Quattara.
Hatua hiyo ya Baraza la Katiba ilimpunguzia Quattara kiasi cha kura 600,000, sawa na asilimia 12 ya kura zote zilizopigwa.