SIKU takriban tisa baada ya Dar es Salaam kutikiswa na milipuko ya mabomu na makombora katika kikosi cha Jeshi cha 511 ambacho ni Ghala Kuu la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Gongo la Mboto, askari zaidi ya 30 wa kikosi hicho wanadaiwa kupiga raia.(Pichani raia wenye majeraha wakionyesha waandishi wa habari jinsi walivyojeruhiwa bila hatia).
Askari hao inadaiwa waliwapiga raia hao usiku wa kuamkia jana kwa madai ya kulipiza kisasi baada ya mwenzao kupigwa na raia wa eneo hilo.

Kwa mujibu wa wakazi hao, tukio hilo lilitokea saa 6.45 usiku, ambapo walishuhudia kundi la askari hao likipita kuanzia mwanzo wa eneo hilo na kumpiga raia yeyote waliyekutana naye barabarani.

Waliokumbwa na shambulizi hilo na kujitambulisha kwa waandishi wa habari kwenye kambi ya waathirika wa milipuko ya mabomu, eneo la Mzambarauni jana, ni Mazoea Nassor, Mohammed Selemani, Rashid Abdallah, Kassim Mango, Andrea Mbezi na bondia maarufu nchini, Mada Mauggo, wote wakazi wa eneo hilo.

Raia hao walioonekana kuwa na majeraha sehemu mbalimbali za miili yao, walidai kuwa mbali na kupigwa pia waliwaporwa simu na fedha mbalimbali pamoja na kumwaga vyakula vya mama lishe, wakati wakiendelea na mashambulizi.

"Wametupora simu na fedha huku wakitupiga mateke, mikanda na ngumi. Wanadai kuwa wamefanya hivyo baada ya mmoja wao kupigwa na raia kwenye kituo cha mabasi cha Gongo la Mboto," amesema Mauggo na kuendelea:

"Mimi nilikuwa nimeshuka kwenye gari langu baada ya kuliegesha, lakini ghafla niliona kundi la wanajeshi wakipita huku wakipiga wananchi. Nikatoa simu kutaka kutoa taarifa Polisi, lakini kabla sijasema lolote nikashitukia nimepigwa mkanda mkononi na kuporwa simu na askari hao," amedai Mauggo.

Kwa mujibu wa Mauggo, baada ya tukio hilo, walikwenda kituo cha Polisi Gongo la Mboto kutoa taarifa, lakini hawakukuta askari kwani nao walikimbia kutokana na tukio hilo na kukiacha kituo wazi.

Amesema, walikwenda kituo cha Sitaki Shari na kufungua jalada namba STK/RB/3030/11 na jalada hilo kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi ambako walitoa maelezo zaidi.

Msemaji wa Jeshi hilo, Luteni Kanali Kapambala Mgawe, alipoombwa na gazeti hili kuzungumzia tukio hilo, alisema wakati huo hakuwa na taarifa za tukio kama hilo na kuahidi kuzifuatilia.

"Bado sijapata hizo taarifa. Lakini nakuahidi nitafuatilia baada ya taarifa yako hii,” alisema Mgawe.

Milipuko ya mabomu ya Gongo la Mboto ilisababisha vifo vya watu zaidi ya 20 na wengine zaidi ya 300 kujeruhiwa na nyumba kadhaa kubomoka.

Tukio hilo limekuja huku baadhi ya raia wakiwa bado hawana makazi, wengine wakiugulia majeraha na baadhi yao wakiendelea kuomboleza kupoteza ndugu zao.