KUTOKANA na hali ya kisiasa kuendelea kuzorota nchini Libya, Serikali ya Tanzania imeamua kuwarejesha nyumbani raia wake waliopo nchini humo.

Utaratibu wa kurejesha Watanzania hao unafanyika kwa kushirikiana na Serikali ya Kenya kupitia ubalozi wake nchini humo. Tanzania haina ubalozi Libya.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, amewaambia waandishi wa habari Dar es Salaam , kwamba Serikali imekuwa ikifuatilia hali ya usalama wa Watanzania hao na Ubalozi wa Kenya umesaidia kuwasajili.

Kwa mujibu wa Membe, baadhi ya wanafunzi wa kitanzania walioko Libya waliomba Serikali iwarudishe nyumbani na itafanya kila liwezekanalo kuhakikisha wote wanaotaka kurejea nyumbani wanafanya hivyo.

“Hivi leo saa 12 jioni, ndege ya Kenya inatua Tripoli na wako baadhi ya Watanzania wataondoka katika kundi hilo la kwanza kurejea nyumbani kupitia Kenya.

“Waambata wetu wawili waliopo katika ubalozi wetu Cairo (Misri) wamekuwa wakizungumza na Watanzania hao kila siku, ili kuhakikisha wanapata msaada wanaohitaji kutoka serikalini,” amesema leo.

Membe amesema, Watanzania waliopo Libya si wengi, wamo wanafunzi 22 na wananchi wengine sita walioko mji mkuu, Tripoli, ambao tayari wamesajiliwa na wapo salama ila tatizo ni ukosefu wa huduma muhimu na hali tete ya usalama nchini humo.

Waziri Membe amesema, alizungumza na Balozi wa Libya nchini, ambaye alikiri kuwa hali ni ngumu, lakini inaweza kudhibitiwa na kwamba maeneo ya Magharibi mwa nchi hiyo na vijijini, hali ni salama.

Amesema alimhakikishia Balozi huyo kuwa wanafunzi wa kitanzania wanaorudi nyumbani wamezingatia hali ya usalama kutokuwa nzuri.

Aliongeza kuwa hali hiyo ikikaa sawa, wanafunzi hao watarejea kusoma na kumwomba Balozi huyo aviombe vyuo vya nchi hiyo vikubali kuwapokea wanafunzi hao hali itakapokuwa shwari.

Kwa mujibu wa Membe, mtikisiko huo ndani ya Serikali ya Libya umetokana na wananchi kutaka mabadiliko ya kidemokrasia, kiuchumi na kukiukwa kwa haki za binadamu.

Amesema pia Serikali ya Tanzania imekuwa makini kutoa kauli ili isihatarishe maisha ya Watanzania walioko katika nchi zenye migogoro hivi sasa, kama Libya, na kuwataka Watanzania kutanguliza uzalendo wanapotoa kauli au maoni kuhusu mgogoro huo.

Wakati huo huo, Waziri Membe alisema jopo la marais watano na mwakilishi wa Ushirikiano wa Kiuchumi wa Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) wako katika mchakato wa kufikia muafaka wa mgogoro wa Ivory Coast.

Membe alisema kuanzia Februari 28, jopo hilo litakutana na Baraza la Amani la Afrika, ili kutoa mapendekezo yao kabla ya kwenda Abidjan kutoa tamko lao.

Waziri alikiri kuwa kuna kazi na changamoto kubwa katika utatuzi wa mgogoro huo, lakini akaongeza kuwa mchakato huo utakapokamilika, suluhisho la mgogoro huo litapatikana.