KAMBI ya Upinzani Bungeni imesema, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange wanapaswa kujiuzulu ili kuwajibika kisiasa kutokana na milipuko iliyotokea katika kambi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Gongo la Mboto, Dar es Salaam.
Kambi hiyo pia inataka maghala yote ya kuhifadhia silaha yahamishwe kutoka kwenye makazi ya raia na kuzihifadhi katika kambi za JWTZ zilizo mbali na makazi hayo.
Kambi hiyo imesema, Dk. Mwinyi na Mwamunyange wanapaswa kujiuzulu ili kupisha uchunguzi huru kuhusu chanzo cha milipuko hiyo iliyoua zaidi ya watu 17.
Msemaji wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa wa kambi hiyo, Joseph Selasini amesema, viongozi hao walikuwa katika nyadhifa hizo wakati wa mabomu yalipolipuka katika kambi ya JWTZ Mbagala, Dar es Salaam,waliahidi kwamba maafa kama hayo yasingetokea tena, lakini yametokea, hivyo wanapaswa kujiuzulu.
“Inaelekea, kwa hiyo kwamba,ahadi yao ilikuwa si ya kweli au hawakuhakikisha kwamba inafanyiwa kazi ili iwe ya kweli. Viongozi hawa hawana budi kuwajibika kwa hiyari yao wenyewe au kuwajibishwa kama itahitajika”amesema Selasini wakati anazungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma.
Waziri huyo kivuli wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, amesema, huu ni wakati mwafaka kwa Dk. Mwinyi na Mwamunyange kujiuzulu nafasi zao ili kuonesha uadilifu wao.
“Si jukumu letu kuwalazimisha wajiuzulu lakini wasipofanya hivyo wananchi wa Tanzania watajua ni watu wa aina gani katika jamii”amesema mwanasiasa huyo muda mfupi baada ya Spika wa Bunge, Anne Makinda kuahirisha kikao cha Bunge kwa sababu ya milipuko hiyo.
Kwa mujibu wa Selasini, kujiuzulu haina maana kwamba umefanya kosa, hivyo Dk. Mwinyi na Mwamunyange waachie ngazi kwa niaba ya wasaidizi wao.
“Wasipojiuzulu sisi kama kambi ya Upinzani hatuwezi kwenda mahakamani, hatuwezi kuwalazimisha lakini Watanzania wanaona na wataamua”amesema na kubainisha kwamba, wana taarifa kwamba milipuko ya jana imeua watu 20, na watu wengi wamejeruhiwa.
Kambi ya Upinzani Bungeni imesema, milipuko ya Gongo la Mboto inaonesha kuwa Serikali haikujifunza lolote kutokana na maafa ya Mbagala takribani miaka miwili iliyopita na kwamba hadi leo Bunge na wananchi hawajaelezwa chanzo cha maafa ya Mbagala, Dar es Salaam.
“Hadi leo hii wananchi au wawakilishi wao bungeni hawajaambiwa kama kulikuwa na makosa ya makusudi au ya uzembe na kama hatua zozote za kinidhamu au za kisheria zilizochukuliwa dhidi ya mtu yeyote kutokana na kusababisha au kuwajibika kwa maafa hayo” amesema Selasini.
“Iko wapi ile ripoti ya Mbagala, wamechunguza wenyenye na ripoti wamekaa nayo”amesema Mbunge huyo wa Rombo mkoani Kilimanjaro.
Kambi hiyo imependekeza iundwe kamati teule ya Bunge la Tanzania au tume huru ya uchunguzi ili kuchunguza kwa kina chanzo cha milipuko hya Gongo la Mboto na madhara yaliyosababishwa.
“Kwa kuzingatia historia ya uchunguzi wa milipuko ya Mbagala mwezi Aprili 2009, Tume Huru au Kamati Teule ya Bunge lazima itoe taarifa yake hadharani kupitia Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania”amesema.
Selasini amesema, milipuko ya Gongo la Mboto inastusha na kusikitisha hasa kwa kuzingatia kwamba haijapita miaka miwili tangu mabomu yalipuke katika ghala la kuhifadhia silaha kwenye kambi ya JWTZ, Mbagala.
Kambi hiyo imesema, gharama za kuzihamisha kambi za jeshi kutoka katika maeneo wanapoishi raia ni gharama za maendeleo hivyo si busara kwa maghala ya kuhifadhia silaha yakaendelea kuwepo jirani na makazi ya raia.
“Haiwezekanikwa serikali kuendelea kuweka maghala ya silaha katika kambi za jeshi zilizo karibu na wananchi na hivyo kuhatarisha maisha yao namna hii” amesema.
“Kwa hiyo Serikali isiogope gharama, hiyo ndiyo gharama ya maendeleo” amesema na kubainisha kwamba, kama maghala ya silaha yasipohamishwa kutoka katika makazi ya raia, upo uwezekano wa watu kufa kutokana na milipuko katika kambi za Changanyikeni, Lugalo, na Kurasini zote za Dar es Salaam.
Kambi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), imetoa pole kwa ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania kwa ujumla kutokana na maafa ya Gongo la Mboto.
Kambi hiyo imezitaka mamlaka zote za umma zinazohusika kuhakikisha kwamba waathirika wa maafa hayo wanapatiwa huduma zote wanazohitaji ikiwa ni pamoja na maziko, matibabu kwa waliojeruhiwa na hifadhi kwa waliopoteza makazi.
Selasini amesema, kwa mujibu wa wataalamu, mabomu yanaweza kulipuka kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kwisha kwa muda wa mabomu husika.
Amesema, mabomu pia yanahitaji kukaa kwenye joto la aina Fulani ni hivyo joto likizidi yanaweza kulipuka.
0 Comments