MAKOMBORA yaliyolipuka juzi usiku katika kambi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kikosi cha 511 kilichopo Gongo la Mboto, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, yamethibitika kuua watu 26, kujeruhi zaidi ya raia 300, kuharibu majengo na magari matano ya Jeshi hilo likiwamo lililosheheni silaha nyingine.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mkuu wa Kikosi hicho, Kanali Aloyce Mwanjile kwa Rais Jakaya Kikwete, aliyezuru kambi hiyo jana mchana kujionea hali halisi, maghala 23 yaliyokuwa na makombora ya aina tofauti yenye uwezo wa kuruka kilometa 22 yanapolipuliwa kitaalamu, yaliteketea.
Kanali Mwanjile alimweleza Rais kuwa mlipuko huo ambao chanzo chake hakijajulikana, ulianzia kwenye ghala namba tano na kusambaa kwa haraka kwenye maghala mengine na hivyo kusababisha athari kubwa kwa Jeshi na wananchi wa maeneo ya karibu na kambi.

“Tunamshukuru Mungu kwa sababu wanajeshi wote na walinzi wa maghala yaliyolipuka wako salama. Tunafanya utaratibu wa kuondoa mabomu yaliyosambaa kwenye makazi ya watu, pamoja na vipande vya mabomu hayo ili kuhakikisha usalama zaidi wa raia wetu waliojawa na hofu,” alieleza.

Aliyataja maeneo yaliyotapakaa mabaki ya mabomu hayo ambayo Jeshi hilo limehadharisha kuwa yanaweza kulipuka wakati wowote endapo yatachezewa au kugongwagongwa kuwa ni ya karibu na kambi hiyo (Gongo la Mboto), Ukonga, Kitunda, Pugu Kajiungeni, Yombo na Tabata,
na hivyo kuwataka wakazi wa maeneo hayo kutoyagusa hadi kikosi maalumu cha Jeshi hilo kitakapoyaondoa.

Naye Mnadhimu Mkuu wa Jeshi hilo, Luteni Jenerali Abdulrahman Shimbo, alisema kombora lililokwenda umbali mrefu zaidi ni lililotua Tabata, kilometa 10 kutoka kwenye kambi hiyo na kuongeza kuwa walijitahidi kwa kadri ya uwezo wao kuhakikisha hadhari zote za kijeshi zinachukuliwa kuzuia hali hiyo kutokea siku tatu kabla ya tukio hilo, walipokagua mabomu hayo.

“Nawahakikishia kuwa hali sasa ni shwari na hakuna makombora mengine yatakayolipuka. Tumeandaa ripoti yetu na kuikabidhi kwa kiongozi wetu ili aipitie, tutaitolea taarifa wakati wowote, lakini ninachotaka mfahamu ni kwamba tulikagua maghala yetu siku tatu kabla ya tukio na kujiridhisha kuwa yako salama, sasa hili lililotokea, tutalitolea maelezo baada ya kuchunguza chanzo,” alisema.

Alisisitiza kuwa milipuko hiyo ni tofauti na ya Mbagala ya Aprili mwaka juzi iliyoua watu zaidi ya 20, kwa sababu hakukuwa na watu waliokuwa wakifanya kazi kwenye maghala hayo wakati ulipotokea.

Kikwete atoa pole
Rais Kikwete aliwataka waliohama makazi yao kutokana na tukio hilo, warejee kwa amani na utulivu kwa kuwa hali ya hatari imekwisha.

Wakati wa mkutano na waandishi wa habari kambini hapo baada ya kutembelea eneo la tukio, Rais Kikwete alisema kilichotokea ni janga la kitaifa, lakini haimaanishi kuwa hali ya usalama ni mbaya.

Aliwapa pole wafiwa na majeruhi na kusema Baraza la Usalama wa Taifa litakutana ili kujua nini kifanyike baada ya tukio hilo.

“Baraza la Usalama litakutana mchana huu (jana) kujadili suala hili na kupanga nini kifanyike baada ya tukio hili, taarifa zitakuwa zikitolewa na viongozi wa Jeshi, ili wananchi wajue kinachoendelea … hali sasa ni shwari, wananchi warejee makazi yao,” alisema Rais Kikwete na kuwataka wananchi kutosikiliza ‘redio mbao’ kwani taarifa zitatolewa na vyombo vya usalama.

Waliokufa na majeruhi
Majeruhi zaidi ya 333 wanaendelea kupokewa katika hospitali za Temeke, Amana na Muhimbili wakiwamo waliovunjika, kuungua na wengine kukatika viungo na baadhi yao walipewa huduma na kuruhusiwa.

Hata hivyo, wakazi wengi wa Gongo la Mboto na maeneo ya jirani, wamejikusanya kwa wingi katika hospitali hizo wakitafuta ndugu zao huku wengine wakishindwa kufahamu walipo.

Kadhalika Rais Kikwete alifika Amana na Muhimbili na kuwapa pole majeruhi hospitalini humo.

Akitoa taarifa kwa Rais Kikwete, Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Amana, Dk. Grace Maghembe, alisema jana asubuhi kuwa hospitali hiyo ilipokea majeruhi 176 wanaume 71 na wanawake 105 na waliovunjika na kukatika viungo waliwapeleka Muhimbili.

Dk. Maghembe alisema wananchi 12 walipoteza maisha eneo la tukio, na mmoja hospitalini hapo na maiti wote walipelekwa Muhimbili ili kuhifadhiwa, ambapo hadi sasa katika hospitali hiyo wapo wagonjwa 15 na 113 wakiwa wamepewa matibabu na kuruhusiwa.

Hata hivyo, takwimu za Dk. Maghembe juu ya idadi ya maiti zinatofautiana na zilizobandikwa kwenye mbao za matangazo hospitalini hapo, zikionesha kupokewa majeruhi 162 na maiti 19.

Kwa mujibu wa karatasi hiyo waliokufa ni Zahalidi Imamu, Neema Nyagiongo (28), Tina Nyagiongo, Stella Nyagiongo, Ally Chambuso (48), Khadija Ally (32), Sophia Salum (55), Hansi Hassan (19), Ally Ibrahim (50), Neema James (14), Vivian Juma (28), Mainda Ismail, Rose Anthony (28), Amina Kihiyo (37), Nasra Salum (28), Somoe Musa (30), Muhidin Mamlo (51) na wawili ambao hawakufahamika majina.

Ofisa Uhusiano wa Muhimbili, Aminiel Aligaesha, alisema maiti watano walipokewa hospitalini huku majeruhi wakifikia zaidi ya 80, kati yao 44 walipelekwa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) kwa matibabu zaidi.

Alitaja maiti wawili kuwa ni Zainab Mohamed na mtoto wa miaka 10 ambaye kabla ya kufariki dunia, alitaja jina la Baba Laiya na majina mengine kutofahamika.

Katika Hospitali ya Temeke, Kaimu Mganga Mkuu, Dk. Mariam Maliwah, alisema jana asubuhi saa 2:48 alipokea majeruhi 74 na maiti wawili.

Alisema katika majeruhi hao, wanne walipelekwa Muhimbili, watano wamelazwa wakiwamo wajawazito wanne na mtoto ambao wana majeraha madogo.

Aliwataja waliokufa kuwa ni Mwanahawa Mohamed (65) na Ally Nginye (74) na majeruhi 34 waliruhusiwa baada ya matibabu.

Mtoto Ramadhan Sultan (11) mkazi wa Gongo la Mboto aliyeungua mguuni kwa bomu, anawatafuta ndugu zake baada ya kupotezana nao juzi wakati akikimbia kutafuta usalama.
Amelazwa Amana na alisema alikuwa anaishi na bibi yake wakati mama na baba yake wakiishi Pugu Majohe ambako alikuwa akikimbilia na mdogo wake, Nurdin Isihaka (10) na kupigwa na bomu mguuni na kuanguka.

Taarifa ya Polisi
Kwa mujibu wa Msemaji wa Polisi, Mrakibu Msaidizi Advera Senso, taarifa za awali zinaonesha kuwa milipuko hiyo imesababisha madhara makubwa vikiwamo vifo, majeruhi, uharibifu wa mali na watu kupotea.

Senso alisema idadi ya watu waliokufa na majeruhi hao imetolewa na hospitali za Muhimbili, Amana na Temeke na kwamba waathirika waliokimbia makazi yao, wamehifadhiwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Sabasaba, vituo vya Polisi Tazara, Buguruni na Msimbazi.

Alisema wananchi wasisikilize uvumi wa watu wanaodai mabomu yanaendelea kulipuka na warudi kwenye makazi yao kwa ajili ya usalama wao na mali zao, kwa kuwa hakuna mlipuko mwingine utakaotokea.

“Wananchi wawe watulivu, warudi kwenye makazi yao na kuendelea na kazi zao kama kawaida, kwa sababu hali hiyo imeshadhibitiwa kwa sasa na hakuna milipuko inayoendelea,” alisema Msemaji huyo.

Aidha, aliwataka wananchi watoe taarifa kupitia namba 0782114515, 0783260334, 0774039029 na 0755756410, endapo wataona kitu wanachokitilia shaka, kwa kuwa kuna mabomu mengine ambayo hayajalipuka na yameruka hadi kwenye makazi ya watu.
Waliokimbia makazi

Watu zaidi ya 4,000 wakiwamo watoto 179 walilazimika kukimbia makazi yao na kulala katika kambi ya muda kwenye Uwanja wa Uhuru, Temeke.

Gazeti hili lilifika uwanjani hapo jana asubuhi na kujionea maelfu ya watu wakihaha kutokana na kupoteza watoto, ndugu, jamaa na marafiki huku wengine wakiwa wamevaa khanga tu na wengi wao wakiwa hawana viatu.

Akizungumzia hali hiyo, Mkurugenzi wa Maendeleo wa Chama cha Msalaba Mwekundu, Julius Kejo, alisema kati ya watoto 179 waliolala uwanjani hapo, 88 wametambuliwa na wazazi wao na kuchukuliwa, huku 91 wakiendelea kupewa huduma muhimu wakisubiri wazazi na ndugu
zao kuwachukua.

Kejo ambaye pia ni Msimamizi wa Shughuli za Chama hicho uwanjani hapo, alisema wamekuwa wakiendelea kutoa huduma ikiwamo kujenga mahema ya kuwahifadhi waathirika na tayari kimewapa huduma ya kwanza watu 47 na wengi wao wamekuwa wakianguka na kupoteza fahamu.

Alisema baada ya tukio hilo, Serikali ilielekeza watu ambao hawana makazi waende hapo ili kurahisisha kuwasaidia waathirika kwa kuwapa huduma ya kwanza na mahitaji muhimu.

Alisema jana asubuhi waliwapa watoto hao maji, juisi na uji; na watu wazima wengi walianza kuondoka saa 11 alfajiri na kwa wasiokuwa na nauli, walibaki wakisubiri msaada wa kurejea kwao.

Alisema watoto walio eneo hilo wanatoka Yombo Vituka, Makangarawe, Ukonga, Gongo la Mboto, Pugu, Kinyerezi, Tabata, Chanika na Majohe, ambapo pia wazazi wamekuwa wakimiminika uwanjani hapo kuendelea kutafuta na kutambua watoto wao.

Kejo alisema kulingana na maelezo waliyopata kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, kuna uwezekano mkubwa wa watu kuendelea kulala uwanjani hapo ambapo ofisi hiyo ilitoa mahema 100 kwa ajili ya hifadhi huku Chama cha Msalaba Mwekundu kikiwa kimejenga 10 na mengine 60
yakiwa mbioni kujengwa.

Akizungumza uwanjani hapo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni, alisema Serikali ilipokea taarifa hiyo kwa masikitiko na baada ya tukio walijipanga na kutenga hospitali maalumu kwa ajili ya kupokea majeruhi na kutoa huduma za tiba bure.

Kauli za waathirika
Wakizungumza na gazeti hili, baadhi ya waathirika walisema hali ya juzi usiku ilikuwa ya hatari na ilisababisha wengi wao kupotezana na familia zao kutokana na kila mmoja kutaka kuokoa roho yake.

Mary Ambakise anayeishi Kipunguni Mashariki alifika uwanjani hapo akilia kwa uchungu, akidai kupotelewa na watoto wake watatu lakini baadaye, alipata wawili na mwingine akiwa hajulikani aliko.

Alisema usiku wakijiandaa kulala, walisikia kishindo kama mlipuko, wengine wakidhani majambazi, lakini hali ilipozidi kuwa mbaya, walitoka kila mmoja akitokomea kusikojulikana na baadaye alijikuta Mbagala, lakini bila watoto wake.

Musa Juma aliyekuwa amebeba mtoto wa kaka yake wa miezi sita, alisema baada ya kusikia mlipuko huo, kila mmoja alikwenda na njia yake, huku yeye akiondoka na mtoto huyo, lakini mpaka wakati huo, hakujua shemeji yake wala kaka yake na wadogo zake wawili waliko.

Mkazi wa Ukonga Mombasa, Shania Abdallah, alikuwa akilia kwa uchungu na kulieleza gazeti hili kwamba amepotelewa na watoto wake wawili, wa miezi minane na mwingine wa mwaka mmoja na miezi saba, na kwamba hadi jana mchana, alishazunguka katika vituo tofauti vya Polisi na uwanjani hapo, bila mafanikio.

Amina Majid alieleza kwa masikitiko jinsi kaka yake alivyojeruhiwa, akisema alikuwa Tazara na aliposikia tukio hilo, akakumbuka kuwa kuna watoto wake nyumbani; akaamua kuchukua pikipiki kuwahi, lakini wakiwa njiani walipata ajali na dereva kufa papo hapo, huku kaka yake akiwa ameumia na kulazwa MOI.

Safari za ndege
Safari za ndege ndani na nje ya nchi ambazo zilizuiwa kuanzia saa 3.15 usiku juzi, zilianza tena jana saa saba mchana, baada ya maofisa wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TAAA), Mamlaka ya Viwanja vya Ndege na maofisa wa Jeshi, Polisi na Usalama wa Taifa, kuridhika kuwa hali ni shwari kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam ambao ulifungwa.

Ofisa Habari wa TAAA, Abel Ngapemba, alilieleza gazeti hili kuwa safari hizo zilianza tena baada ya maofisa wa vyombo hivyo kukagua uwanja huo juzi saa sita usiku na jana asubuhi hadi mchana, na kuridhika kuwa hali ya uwanja huo ni shwari na safari za ndege zinaweza kuanza tena.

“Tuliokota vipande vikubwa vinane vya mabomu na vidogo 16, lakini vyote vilishateketea. Kwa hiyo, hali ni shwari na kuanzia saa saba hii, wasafiri wameanza kukaguliwa kwa ajili ya kwenda kupanda ndege ili safari zianze,” alisema Ngapemba.

Inakadiriwa kuwa abiria takriban 1,000 waliathiriwa kutokana na kusimamishwa kwa safari hizo za ndege kuanzia juzi usiku na miongoni mwa ndege zilizoathirika ni KLM, Swiss Air, Egypt Air na ndege za nchini.

Bunge laomboleza
Spika wa Bunge, Anne Makinda, alilazimika kuvunja kikao cha saba cha Mkutano wa 10 wa Bunge ili wabunge hao waungane na Watanzania wengine kuomboleza na kusaidia waathirika.

Makinda alisema hayo muda mfupi baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kutoa tamko juu ya ajali hiyo ambalo alieleza kuwa aliiagiza JWTZ kuunda baraza haraka iwezekanavyo kwa ajili ya kuchunguza chanzo cha milipuko hiyo na hatua stahili za kuchukuliwa.

“Nimekuwa nikipokea taarifa kuhusu tukio hilo hadi saa 11 alfajiri, na leo (jana) Rais Kikwete ameitisha mkutano wa dharura na Baraza la Usalama wa Taifa lengo likiwa ni kujadili nini cha kufanya,” alisema Pinda.

Waziri Mkuu alisema kikao hicho cha dharura kilichoitishwa na Rais pia kitawajumuisha Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi na Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo.

Ushauri wa CUF
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, mbali ya kumtaka Dk. Mwinyi na Mwamunyange wajiuzulu, amemtaka pia Amiri Jeshi Mkuu, Rais Kikwete kuwahakikishia wakazi wa Dar es Salaam kuishi bila hofu kutokana na matukio yanayoendelea kujitokeza ya milipuko katika kambi za Jeshi.

“Tunamsihi Waziri Mwinyi kulinda heshima yake kwa kufuata nyayo za baba yake Mzee Ali Hassan Mwinyi alipokuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, alipojiuzulu kutokana sakata la mauaji mkoani Shinyanga,” alisema Profesa Lipumba katika taarifa hiyo ya CUF.

CCM yaomboleza
CCM imeiomba Serikali ichukue hatua za haraka za kusaidia wenye kuhitaji msaada wa maeneo ya kuishi, matibabu na huduma nyingine za mahitaji ya kibinadamu, ikiwa ni hatua ya dharura na baada ya hapo, kufanya tathimini ya haraka iwezekanavyo ili wanaostahili fidia, wapate mapema na kurejea katika maisha yao ya kawaida.

Bilal atembelea eneo
Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal alitembelea Kikosi hicho ambako alipata maelezo ya namna mabomu hayo yalivyolipuka na hasara iliyopatikana.

Akizungumzia tukio hilo, Kanali Mwanjile alimweleza Makamu wa Rais kuwa jitihada zinafanywa na wataalamu wa Jeshi hilo kwenda maeneo ambayo mabomu hayo yanadaiwa kutapakaa ili kuyaondoa.