Rais Jakaya Kikwete, amesema ana imani mgogoro wa kisiasa ulioikumba Ivory Coast baada ya kufanyika kwa uchaguzi, utamalizika kwa kuwa nchi nyingi za Afrika zinataka kuona viongozi wanaingia madarakani kwa njia ya kidemokrasia.
Aliyasema hayo jana alipohutubia kikao cha Wakuu wa Nchi na Serikali kilichofanyika nchini Ethiopia na hotuba yake kupatikana jijini Dar es Salaam.

Rais Kikwete alisema Afrika inahitaji kuwa huru kidemokrasia na kwamba nchi nyingi za Afrika hivi sasa zinafanya uchaguzi kwa kufuata demokrasia ingawa bado zipo chache zinazokwenda kinyume.
Hata hivyo, alisema wananchi wa nchi hizo wana haki ya kuchagua kiongozi wanayemtaka kwa uhuru na haki.
Aliongeza kuwa viongozi wanaoingia madarakani bila kufuata demokrasia, watafutwa uanachama wa Nchi za Afrika.
Aliwataka viongozi wa Afrika kukubali matokeo yanayopatikana kwa njia ya wananchi kupiga kura na kwamba wale wanaoyakataa wanakuwa wanapingana na sauti ya umma.
Alisema demokrasia katika nchi nyingi za Kiafrika itachukua muda mrefu kustawi na kwamba lazima maadili yazingatiwe katika kuijenga ili kuheshimu utawala wa sheria.
Aliwaambia viongozi hao kuwa ni lazima utawala wa sheria uzingatiwe na haki za binadamu zilindwe ili kuwawezesha wananchi kufurahia uhuru, kupata fursa ya kuabudu na vyama vya kiraia kuwa huru.
Alisema ikiwa utawala wa sheria, utawala bora na demokrasia vitakosekana katika nchi za Kiafrika, kutasababisha kudumaza maendeleo ya wananchi wa nchi hizo na kuwafanya wabaki nyuma kiuchumi.
Rais Kikwete alisisitiza kwamba nchi nyingi za Afrika bado ni changa kisiasa na hivyo si kila kitu kinachofanywa kinakuwa sahihi na kuongeza kuwa ikiwa maadili ya Kiafrika yatazingatiwa, kutasaidia kuwepo ustawi wa kijamii.