Serikali imeitaka Baraza la Majadiliano ya pamoja katika Utumishi wa umma kuhakikisha mwafaka unapatika kuhusiana na nyongeza ya mishahara kwa wafanyakazi kama inaendana na hali halisi ya uchumi wa nchi.
Rai hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma), Hawa Ghasia,(Picani juu) wakati akizindua Baraza la pili la majadiliano ya pamoja ambapo alisema kuwa
anatarajia baraza hilo litafikia mwafaka wa kukubaliana na nyongeza ya mshahara kama itakuwa inakidhi maslahi ya watumishi wa umma au la.Ghasia alisema uzoefu uliopatika katika baraza la kwanza umeonyesha changamoto kubwa katika kuainisha maslahi ya watumishi pamoja na uwezo mdogo wa bajeti ya serikali inayotokana na kiwango cha ukuaji wa uchumi ambapo mapato ya serikali yamekuwa hayakidhi mahitaji.
Alisema hali hiyo iliathiri utekelezaji wa ushauri mzuri wa Baraza uliotolewa kwa serikali wa kuboresha maslahi ya watumishi wa umma.
Aidha, alisema sehemu kubwa ya watumishi wa umma siyo wazalishaji na kwamba majukumu yao ni kutengeneza mazingira mazuri ambayo yatawawezesha kuzalisha zaidi hasa kwa upande wa sekta binafsi.
0 Comments