Tukio la kushangaza la kuzikwa katika kaburi la pamoja kwa vichanga 10 limetokea jijii Dar es Salaam, huku umma ukipigwa butwaa na hali hiyo.
Hali hiyo iligundulika jana eneo la Mwananyamala Kwa Kopa, karibu na nyumba ya mkazi mmoja aliyetajwa kwa jina la Mariamu Harubu, jirani na makaburi ya Mwananyamala.
Watoto wote walikutwa wamezikwa kwenye jalala la nyumba ya mkazi huyo, wakiwa wamefukiwa chini kina cha futi moja na nusu.
Hali hiyo iliyozua taharuki katika eneo hilo kwa kuvuta kundi kubwa la watu, ilitokea jana mchana, wengi wakiwa hawaamini macho yao miili hiyo ilipochimbuliwa kwenye kaburi hilo.
Mkazi wa jirani na nyumba hiyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema watoto hao walikutwa wakiwa wamevingirishwa kila mmoja katika kanga yake na kufunikwa kwa shuka moja.
Shuda huyo nyeupe ilikuwa na lebo ya Bohari ya Madawa Taifa (MSD) hopitali ya Mwananyamala.
Akiwa eneo la tukio, Daktari wa hospitali ya Mwananyamala aliyetambuliwa kwa jina moja tu la Karamerian, alipoulizwa kukoni kuwako kwa shuka hiyo, alisema suala hilo lipo mikononi mwa polisi na hawezi kusema lolote.
Akizungumza na gazeti hili jana kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa kipolisi wa Kinondoni, Charles Kenyela, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kufafanua kuwa wanaendelea na uchunguzi.
Kamanda Kenyela alisema, Hamudu Mbaga (39), mkazi wa Mwananyamala kwa Kopa alipokwenda kutupa taka katika jalala hilo alikuta limefukiwa ndipo alipohisi harufu kali ikitoka katika shimo hilo.
Alifafanua kuwa baada ya kuanza kufukua aliona miili ya watu na kuamua kwenda kutoa taarifa kwa mjumbe wa nyumba kumi na baada ya hapo walitoa taarifa polisi.
Baada ya polisi kufika eneo la tukio walifukua shimo na kutoa miili ya watoto hao.
Kamanda huyo alisema kuwa kati ya watoto hao 10 waliofukiwa watano ni wa kike na watano ni wa kiume.
Kwa mujibu wa Kenyela, haikuweza kufahamika mara moja watoto hao walifukiwa lini katika jalala hilo.
“Tukio hilo limegundulika leo (jana) saa saba, ambapo watoto hao walikutwa wamefukiwa. Kwa kweli tukio hili ni la kusikitisha sana, lakini bado tunaendelea na uchunguzi ingawa bado tunaendelea kushirikiana na uongozi wa Hospitali ya Mwanayamala ili tuweze kufahamu watoto hao walikotoka,” alisema Kamanda Kenyela.
Alisema polisi bado wanaendela na uchunguzi ili kubaini ni sababu zipi ziliwafanya watoto hao kutupwa na baada ya kukamilika uchunguzi huo watatoa taarifa.
Kenyela alisema miili ya watoto hao imehifadhiwa katika Hospitali ya Mwananyamala kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi.
Hata hivyo, hakuna kiongozi yeyote wa Hispitali ya Mwananyamala aliyekuwa tayari kuzungumsia suala hilo.
Habari zaidi zinasema kuwa miili ya watoto hao ilikuwa haijaaribika sana, hali inayoonyesha kuwa hawakuzikwa siku nyingi.
Kumekuwa na matukio ya vichanga kutupwa ovyo baada ya kuzaliwa na mama zao kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo kisingizio cha kushindwa kulea.
Hata hivyo, haijawahi kutokea kutupwa kwa vichanga vingi kwa mpigo kama ambavyo vimebainika kuzikwa kinyemela Mwananyamala.
0 Comments