Tatizo la maji katika Jimbo la Ubungo linachangiwa na upotevu wa maji njiani wakati yakisafirishwa kutoka kwenye mtambo wa Ruvu, unaosababishwa na kitendo cha kujiunganishia maji kwa njia haramu.
Mbunge wa Jimbo hilo, John Mnyika alibainisha hilo kwenye kongamano la maji lililoandaliwa naye kwa lengo la kujadili sera, sheria na mikakati ya sekta ya maji safi na maji taka-fursa na changamoto kwa wananchi jimboni humo.
Kongamano hilo lilijadili pia hali halisi ya upatikanaji wa maji Ubungo na wajibu wa wadau mbalimbali katika kukabiliana na upungufu huo.
Mnyika alisema mahitaji ya maji jimboni humo, ni karibu lita 450,000, lakini asilimia 50 ya maji yanayosambazwa huishia njiani kutokana na sababu haramu.
“Sababu inayochangia upungufu, ni kitendo haramu cha kujiunganishia maji bila ya kufuata utaratibu unaotakiwa. Kitendo hiki kiko katika sehemu mbili, upande wa Mamlaka yenyewe ya Majisafi na Majitaka (Dawasco) na ule wa wananchi,” alisema.
Alisema viosk vya maji vilivyo na baraka za Dawasco vinavyofanya biashara ya kuuza maji, ndivyo vinavyochangia maji yasitolewe kwa wananchi na mamlaka hiyo na kwamba hali hiyo huenda inafanyika makusudi ili biashara hiyo iweze kuendelea.
Alisema pia kitendo cha baadhi ya wananchi kujiunganishia maji kiholela kwa kutoboa bomba kubwa la maji, kunasababisha maji mengi kupotelea njiani na hivyo kuwa vigumu kuwafikia wananchi wengine wa jimbo hilo.
0 Comments