Mkazi wa Ukonga jijini Dar es Salaam, Sabela Mganga (31), amefariki dunia baada ya kujifungua mapacha kutokana na kuzuiwa na uongozi wa Zahanati ya COH iliyopo Ukonga Mazizini kwenda kupata huduma zaidi Hospitali ya Amana wakimtaka kwanza alipe Sh. 155,800 kama gharama za kujifungua.
Baada ya mwanamke huyo kujifungua, daktari wa zahanati hiyo, Dk. Babu Machondela, alitoa maelekezo mzazi huyo apelekwe Amana kwa ajili ya matibabu zaidi ikiwemo kuongezewa damu, lakini muuguzi mmoja alikataa katakata.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, kaka wa marehemu, Christopher Chakulanga, alisema marehemu alipelekwa katika zahanati hiyo ambayo ni ya mtu binafsi kwa ajili ya kujifungua.
Alisema alipofikishwa katika zahanati hiyo Februari 5, mwaka huu, alijifungua mapacha na baada ya hapo hali yake haikuwa nzuri kutokana na kupungikiwa damu.
Alisema baada ya siku mbili kupita, waliuomba uongozi wa COH wamchukue wampeleke Amana, lakini walikataliwa kwa kuwa walikuwa wanadaiwa.
Aliongeza kuwa awali waliambiwa walitakiwa kulipa Sh. 60,000 kwa ajili ya huduma ya kujifungua, lakini baadaye uongozi wa zahanati hiyo uliwaambia kuwa wanatakiwa walipe Sh. 155,800 kwa siku tatu alizokaa hapo, fedha ambazo walisema hawakuwa nazo na badala yake walikuwa na Sh. 30,000.
Alisema muuguzi huyo alikataa kutoa ruhusa na kudai kuwa hawezi hadi hapo atakapopewa fedha hizo zilizobaki kwani bosi wao haruhusu mgonjwa kuondoka kama anadaiwa fedha za matibabu.
“Kwa kweli walivyonikatalia nisiondoke na mgonjwa wangu niligombana nao kwani hali yake ilikuwa inazidi kuwa mbaya halafu muuguzi alikataa kumruhusu kwa madai kuwa atakatwa fedha hizo katika mshahara wake," alisema Chakulanga.
Chakulanga alisema hali ya marehemu ilizidi kuwa mabaya na walipojaribu kumchukua kwa nguvu kumwingiza kumpeleka Amana, alifariki dunia hata kabla hajafikishwa garini.
Alisema wakati wa purukushani za kutaka kumwondoa mgonjwa huyo, muuguzi mmoja aliwanyang'anya simu mbili ndugu waliokuwa wanamuuguza marehemu.
“Zahanati hii imenihuzunisha sana. Hivi inawezekana kweli fedha hizo zisababishe kutoa uhai wa mtu wakati tulijipanga wanandugu kuchanga tukalipe deni hilo," alisema Chakulanga.
Alifafanua kuwa zahanati hiyo haina huduma ya benki ya damu ila waliendelea kumshikilia mgonjwa huyo huku wakijua hawawezi kumtibu.
Aidha, alisema walipofikisha mwili wa marehemu huyo Hospitali ya Amana, walitakiwa kuonyesha kumbukumbu za alikotokea ili kutambua kifo hicho kilitokana na nini, lakini ndugu waliporudi katika zahanati hiyo kuzitafuta hawakuzipata.
Hata hivyo, licha ya kukosa taarifa kutoka zahanati hiyo, Hospitali ya Amana iliwaambia kwamba marehemu alifariki dunia kutokana na ukosefu wa damu baada ya kujifungua.
Kuhusu shughuli za mazishi, alisema wanatarajia kusafirisha keshokutwa kwenda mkoani Dodoma kwa ajili ya maziko na kwamba watoto waliozaliwa wanaendelea vizuri.
Mmoja wa madaktari waliokuwepo tangu siku ya kwanza ambayo marehemu alifikishwa kwenye zahanati hiyo kwa ajili kujifungua, alisema mwanamke huyo alijifungua salama ila alikuwa anakabiliwa na upungufu wa damu.
Dk. Babu Machondela, alibainisha kuwa matatizo mengine yaliyomkumba marehemu ni kukohoa, shinikizo la damu na kwamba akiwa na ujauzito wa miezi sita, alishaambiwa kuwa akajifungulie Hospitali ya Amana, lakini bahati mbaya hakufanya hivyo.
“Tuliamua kumzalisha kwa sababu walivyomleta tayari mtoto alishaanza kutoka hivyo tukampatia huduma hiyo kwani tusingeweza kumuacha,” alisema Dk. Machondela.
Alisema hatua ya muuguzi wa zahanati hiyo kumkatalia mgonjwa kwenda Amana kwa madai ya kutomaliza deni, si maadili ya kazi.
“Kama mgonjwa hajamaliza deni lake na yuko katika hali mbaya kumng'ang'ania siyo maadili ya kazi kwani ni lazima tujali afya yake kwanza halafu fedha zitafutwe baadaye,” alisema Dk. Machondela.
Alisema ameshindwa kuelewa ni kwanini muuguzi huyo alikataa kumruhusu marehemu wakati tayari alishatoa kibali cha kupelekwa Hospitali ya Amana kwa ajili ya matibabu mengine kwani alikuwa na matatizo mbalimbali.
Dk. Machondela alisema muuguzi huyo atatakiwa kuandika barua na kutoa maelezo ya kina kueleza ni kwanini aliamua kumzuia mzazi huyo wakati alishapatiwa kibali na kwamba maelezo hayo atayapeleka kwa uongozi wa Zahanati kwani yeye hawezi kutoa uamuzi wa mwisho.
0 Comments