Shirika lla Umeme nchini (Tanesco), limetangaza kuongezeka kwa makali ya mgawo wa umeme nchi nzima kutoka siku tatu kwa wiki hadi siku tano.
Akizungumza jana, Meneja Uhusiano wa shirika hilo, Badra Masoud alisema kuongezeka kwa makali hayo kumetokana na kuzidi kupungua kwa kina cha maji katika bwawa la Mtera.
Badra alisema hali hiyo imesababisha kuwa na upungufu wa megawati 230 katika gridi ya taifa.

Alisema katika hali ya kawaida kweny gridi ya taifa kunapaswa kuwa na megawati 702 lakini zilizopo hivi sasa ni megawati 472.
Alisema wakati mgawo unaanza ulikuwa siku tatu kwa wiki lakini mgawo huo umeongezeka makali hadi kufikia siku tano.
Alisema wananchi wengine watapata nishati hiyo kuanzia saa mbili asubuhi hadi 12 jioni na wengine watapata kuanzia muda huo hadi saa saa tano usiku.
Bwawa la Mtera ndilo kubwa tunalolitegemea kulinganisha na lile la Kihansi ambalo lina uwezo mdogo wa kuhifadhi maji kwa hivyo maji yakipungua hakuna namna inabidi tuongeze mgawo,” alisema
Badra alisema hivi sasa shirika hilo linanunua umeme wa megawati 10 kutoka kampuni ya kuzalisha umeme ya IPTL.
Alisema kampuni hiyo inauwezo wa kuzalisha hadi megawati 100 lakini inashindwa kufanya hivyo kutokana na kutokuwa na mafuta.
Tunazungumza na serikali tuone uwezekano wa kuipatia mafuta IPTL ili ianze kuzalisha na nina uhakika itapatiwa mafuta na kuanza uzalishaji kama kawaida,” alisema Badra.
Kuhusu kisima cha kuzalisha gesi cha Pan African Energy kilichopo kisiwani Kilwa, Badra alisema kinaendelea na matengenezo na hakijaanza kuzalisha.
Kufungwa kwa kisima hicho kulisababisha upungufu wa megawati 40 katika gridi ya taifa na kampuni hiyo iliahidi kuwa mwezi huu kitaanza kufanyakazi.
Mgawo huo umekuwa na athari kubwa za kiuchumi kwa wananchi walio wengi na wameendelea kulalamika kuwa unakwamisha shughuli zao za kiuchumi na giza limekuwa likichochea vitendo vya uhalifu maeneo mbalimbali.
Wameitaka serikali itafute mbinu za haraka za kumaliza makali ya mgawo kwani wanapata athari kubwa kwa kukosa umeme.