RAIS Jakaya Kikwete(Pichani) yuko mjini Nouakchott nchini Mauritania, kushiriki katika mkutano wa wakuu wa nchi sita za Afrika waliopewa jukumu la kutafuta suluhisho la kisiasa nchini Ivory Coast.(Kulia kwa raisi ni waziri wetu wa mambo ya nje Mh: Bakari Membe).
Mkutano huo wa kundi la nchi zinazojulikana kama High Level Panel for the Resolution of the Crisis in Ivory Coast utamshirikisha Rais Kikwete na marais wenzake wa Mauritania, Burkina Faso, Chad, Afrika Kusini, Equatorial Guinea ambayo inashikilia uenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) kwa sasa, na Nigeria ambayo ni uenyekiti wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Uchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS).

Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu jana kwa vyombo vya habari, Rais Kikwete aliondoka nchini jana asubuhi, na baada ya kumalizika kwa mkutano huo jana, leo viongozi hao wa nchi sita watasafiri kwenda Abidjan, Ivory Coast ambako watakutana na viongozi hao wawili wa Ivory Coast wanaovutana kuhusu uongozi wa nchi hiyo.

Kundi la nchi hizo sita lilichaguliwa na Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika (AU) uliofanyika mjini Addis Ababa, Ethiopia, mwezi uliopita kutafuta suluhisho la mzozo wa kisiasa katika Ivory Coast ambao ulizuka baada ya Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo uliofanyika Novemba 29, mwaka jana.

Kura zilizopigwa katika raundi ya pili ya Uchaguzi Mkuu huo kati ya aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Alassane Quattara, na Rais Laurent Gbagbo, Quattara alitangazwa kuwa mshindi na Tume Huru ya Uchaguzi kwa kupata asilimia 54.1 kulinganisha na asilimia 45.9 za
Gbagbo aliyekuwa anatetea kiti chake.

Matokeo hayo yalithibitishwa na Ujumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika Ivory Coast,
uliopewa jukumu la kusimamia na kuhakikisha unafanyika uchaguzi huru na wa haki nchini humo kulingana na Makubaliano ya Linas-Marcoussis ya mwaka 2004 na, kwa mujibu wa Makubaliano ya Kisiasa ya Ouagadougou ya mwaka 2007.

Matokeo hayo pia yanakubaliwa na jumuiya ya kimataifa, Umoja wa Ulaya (EU), ECOWAS na AU.

Hata hivyo, Baraza la Katiba la nchi hiyo lilibatilisha matokeo hayo, likafuta matokeo ya kura kutoka majimbo saba ya kaskazini mwa Ivory Coast ambako ndiyo ngome ya Quattara na hatimaye kumtangaza Gbagbo mshindi.

Kutokana na hali hiyo, kila upande ulitangaza Serikali yake hata kama vyombo vya habari vya Serikali, Jeshi, utumishi wa umma na taasisi nyingine nyeti za Serikali zinabakia kwenye udhibiti wa Gbagbo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, mkutano wa jana mjini Noaukchott ungefunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Mauritania, Mohamed Abdel Aziz na viongozi wote sita walitarajiwa kutoa maneno ya ufunguzi.