AY amewataka wasanii kugoma kulipwa fedha kidogo kwenye maonyesho na badala yake wawe na msimamo mmoja katika kupanga viwango vya malipo yao .AY aliyasema hayo wakati akiwasilisha mada kuhusu Harakati za Kuufanya Muziki wa Kizazi kipya kuwa wa kimataifa kwenye Jukwaa la Sanaa linaofanyika kila wiki katika Ukumbi wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ambapo alisema kwamba, wasanii hapa nchini wamekuwa ni wepesi kulalamika wanapolipwa malipo kidogo lakini wagumu kuchukua hatua katika kukomesha hali hiyo.Katika hili alisisitiza kwamba, ni bora msanii akubali kulala njaa kwa siku moja ili aweze kula kwa mwaka mzima badala ya ilivyo sasa ambapo wamekuwa ni wa kulilia fedha za kukidhi matatizo yao madogomadogo tu.

“Huko Nigeria kulikuwa na mchezo kama huu wa wasanii kulipwa fedha ndogo kwenye maonyesho lakini kuna siku wasanii wote waliamua kugoma kushiriki shoo za nyumbani hadi hali itakapobadilika. Leo hii msanii wa Nigeria analipwa dola laki moja na nusu hadi laki mbili wakati hapa kwetu ni ndoto” alisisitiza AY huku akiwaomba wasanii kuwa na umoja katika hili.