Hospitali ya Burhani ya jijini Dar es Salaam, imetangaza kutoa huduma ya operesheni za macho kwa wagonjwa 100, itakayotolewa bila malipo kwa siku nne mfululizo, kuanzia Jumatatu ya wiki ijayo.
Kwa mujibu wa uongozi wa hospitali hiyo, huduma hiyo itatolewa ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya kusherehekea Sheikh wao, Mtukufu Dk. Syedna Mohamed Burhanuddin Saheb (TUS), kutimiza umri wa miaka 100
Hospitali ya Burhani inafanya operesheni za macho bure kusherehekea miaka mia moja ya Shehe wao Mtukufu Dk. Syedna Mohamed Burhanuddin Saheb (TUS) kuanzia tarehe 7/2/2011 hadi 10/2/2011,” ilieleza sehemu ya taarifa ya uongozi wa taasisi hiyo.
Uongozi huo umewataka watu wote wenye matatizo ya mtoto wa jicho (cataract) na presha ya macho (glaucoma), kupitia kwenye vitengo vya macho katika hospitali za Amana, Temeke, Mwananyamala na Amtulabai Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam.
Ulieleza watakaogundulika na matatizo hayo, wataandikishwa majina na namba zao za simu pale pale kwenye kitengo cha macho kwa ajili ya operesheni zitakazofanyika kwenye Hospitali ya Burhani, iliyoko Mtaa wa Kaluta na Morogoro, jijini Dar es Salaam.
Uliongeza kuwa wagonjwa wengine wanaweza kujiandikisha moja kwa moja kwenye Hospitali ya Burhani kwa Maimuna Omary.
Idadi ya wagonjwa watakaochukuliwa ni mia moja. Kwa hiyo watakaowahi kujiandikisha ndio watakaohudumiwa kwanza,” ilieleza sehemu ya taarifa ya uongozi wa hospitali hiyo.