Mwezi mmoja baada ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kutoa noti mpya, Gavana wa Benki hiyo, Profesa Benno Ndulu, amesema tayari kuna wajanja wachache wameanza kughushi noti hizo na kuonya kuwa wakati wowote kuanzia sasa watakamatwa.
Profesa Ndulu alisema hayo alipokuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari, katika ofisi za BoT, jijini Dar es Salaam jana.
Alisema wajanja hao wameanza kutengeneza noti bandia mfano wa noti mpya zilizotolewa na BoT Januari, mwaka huu, kwa kutumia mwanya wa uchache wake katika mzunguko na kwa kutumia pia, udhaifu wa baadhi ya watu kutozijua noti hizo ili kuwatapeli.
“Wajanja wapo na wameanza kutengeneza noti bandia kwa ku-take advantage (kutumia mwanya) kwamba, watu wengi hawazijui noti mpya, sisi tutaendelea kutoa elimu kwa umma,” alisema Profesa Ndulu na kuongeza: “Tunatarajia kuwakamata watu hao.”
Alisema BoT ina mikakati endelevu ya kufikisha elimu “Tambua noti zako” kwa wananchi wote kupitia matangazo, semina, ushiriki katika mikusanyiko mikubwa kama Sabasaba na Nanenane na kwenye masoko pamoja na minada mikubwa ya mifugo.
Maswali ya kujibiwa
Profesa Ndulu alisema swali la kwanza liliulizwa kwamba, noti mpya zikisuguliwa kwenye karatasi nyeupe zinaacha rangi na kwamba zikilowa zinatoa rangi, je, hiyo haitokani na uduni wa noti hizo mpya?
Akijibu swali hilo, Profesa Ndulu alisema hali ya kuacha rangi noti zinaposuguliwa kwenye karatasi nyeupe ni ya kawaida kwa noti zote zilizochapishwa kwa teknolojia maalum inayojulikana kitaalamu kama “Intaglio Printing”.
Gavana huyo alisema aina hiyo ya uchapishaji inazifanya noti kuwa na hali ya mkwaruzo zinapopapaswa na kwamba, teknolojia hiyo imetumika ili kuimarisha kingo za noti kwa lengo la kupunguza uwezekano wa kuchanika na kuchakaa haraka.
Alisema mikwaruzo hiyo huacha rangi noti inaposuguliwa kwa nguvu kwenye karatasi nyeupe kitendo ambacho kinathibitisha kuwa noti hiyo ni halali, pia hali hiyo ni moja ya alama ya usalama inayothibitisha kuwa noti siyo ya bandia.
Vilevile, alisema noti halali hazichuji zikilowekwa kwenye maji kama inavyodaiwa kwa kuwa wino uliotumika hauyeyuki katika maji.
Alisema noti hizo zimetengenezwa kwa tekonolojia ya kuwekewa kinga dhidi ya uchafu inayojulikana kitaalamu kama ‘Anti Soiling Treatment’ ili kupunguza uwezekano wa kunasa uchafu inapokuwa katika mzunguko na kwamba, teknolojia hizo mbili zinalenga kuongeza uhai wa noti katika mzunguko.
Kuhusu swali kwamba, noti za zamani ni halali na zinaendelea kutumika, Profesa Ndulu, alisema noti hizo bado ni halali na zinaendelea kuwa katika mzunguko pamoja na zile mpya mpaka zitakapotoweka kwenye mzunguko kwa sababu za uchakavu wake.
“Kwa hiyo wananchi wanashauriwa kuendelea kutumia noti za toleo la zamani bila wasiwasi wowote … itachukua mwaka mmoja na nusu noti za zamani kuondoka kwenye mzunguko. Hata noti za Dola za Marekani za zamani na mpya zinaendelea kutumika wakati mmoja mpaka sasa,” alisema Profesa Ndulu.
Alisema wataalamu wa nje na ndani, akiwamo Mkemia Mkuu wa Serikali, wamepima utepe uliopo kwenye noti za zamani na kujiridhisha kwamba, hauna uwezo wa kutengeneza kilevi na kwamba, madai hayo yanatokana na imani tu za baadhi ya watu.
Alitoa kauli hiyo kutokana na kuwako na madai mitaani kuwa ‘wabua unga’ hukwangua utepe unaong’aa katika noti na kuunusa kama kilevi cha kuwachangamsha.
Alisema Benki ya NMB, ambayo ina matawi nchi nzima, ndiyo iliyopewa noti mpya nyingi na kwamba, noti zilizotumika kulipa watumishi wake mshahara wa Januari, mwaka huu, zilikuwa ni zile mpya.
Kuhusu swali kwamba noti mpya ni ndogo kuliko za zamani kwa umbo, je, thamani yake siyo pungufu kuliko zile za toleo lililotangulia, alisema thamani ya noti ni ile iliyoonyeshwa kwa tarakimu zilizoandikwa kwenye noti yenyewe bila kujali ukubwa wake, hivyo, akasema thamani ya noti za zamani na za sasa haitofautiani.
Akijibu swali kwamba, kumekuwa na matatizo ya upatikanaji wa noti mpya, je, BoT ina mpango gani kuhakikisha noti mpya zinapatikana nchi nzima, alisema BoT huingiza noti mpya katika mzunguko kupitia benki za biashara na kwamba, inaendelea kutoa noti hizo kupitia benki hizo.
Hata hivyo, alisema kwa kuwa mtandao wa baadhi ya matawi ya benki ni mpana, imechukua muda mrefu kwa baadhi ya maeneo kufikiwa na noti hizo.
Alisema kwa kuwa biashara nchini haina mipaka, noti hizo zitaendelea kusambaa nchini kote kupitia mzunguko wa kibiashara na kuongezeka siku baada ya siku.
Kuhusu swali kwamba, noti halali zina tofauti gani na noti bandia, Gavana Ndulu alisema aliwashauri wananchi kuzichunguza kwa makini noti kwa kutumia alama za usalama kama zilivyoainishwa kwenye matangazo na vipeperushi vilivyotolewa na BoT, ama kuwasiliana na ofisi za benki hiyo kwa ufafanuzi zaidi pale mtu anapokuwa na shaka na noti hizo.
Akijibu swali kwamba, kwa kuwa BoT inabadilibadili fedha kila baada ya miaka mitano hadi saba, je, kwanini isiwe na toleo la kudumu kama ilivyo kwa fedha ya Uingereza au ya Marekani, alisema kubadili noti husababishwa na maendeleo ya teknolojia ya uchapaji wa noti katika kuongeza uhai wa noti katika mzunguko na kuweka alama bora zaidi za usalama ambazo ni ngumu kuzinghushi.
Hata hivyo, alisema sio kweli kwamba Uingereza na Marekani hawajabadili noti zake na kwamba, kuna mabadiliko makubwa na mengi yaliyopita na yanayotarajiwa kwa noti za nchi hizo.
Alisema kubadili noti kunasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza wimbi la utengenezaji wa noti bandia.
Kuhusu swali kwamba, kwa nini BoT haikutoa noti kubwa zaidi ya 10,000 ili kurahisisha malipo katika biashara, Profesa Ndulu alisema BoT haikuona haja ya kutoa noti yenye thamani kubwa zaidi kwa sasa kwani malipo makubwa yanahimizwa kufanywa kupitia njia nyingine za kibenki.
Alisema noti za Sh. 10,000 bado inakidhi mahitaji ya malipo ya kawaida katika biashara kwa sasa.
Profesa Ndulu alisema gharama za uchapishaji noti mpya imepunguza asilimia 30 kulinganisha na noti za zamani.
Akijibu swali kwamba, kutolewa kwa noti mpya kama ni njia ya kudhibiti fedha haramu, alisema hakuhusiani na hilo kwani idadi yote ya fedha zilizoko kwenye mzunguko wanazijua.
Alisema hadi kufikia juzi, akiba ya fedha za kigeni zilizopo, zinafikia dola za Marekani bilioni 3.8, ambazo zinaweza kutumika kwa miezi sita hadi saba kulipa madeni na kununulia bidhaa kutoka nje.
Profesa Ndulu alisema ni Tanzania pekee ndiyo ina kiasi hicho cha fedha katika nchi zote za Afrika Mashariki.
Alisema pia kufikia juzi, akiba ya fedha za kigeni iliyopo katika benki zote za biashara nchini, inafikia dola za Marekani bilioni moja wakati akiba ya fedha za kigeni za Watanzania zilizoko katika mabenki, inafikia dola za Marekani bilioni 1.5.
Umeme kuporomosha uchumi
Akizungumzia athari za uchumi wa nchi kufuatia mgawo wa umeme unaoendelea hivi sasa nchini, Profesa Ndulu alisema mgawo huo utaathiri uchumi wa nchi katika robo ya mwisho (Aprili-Juni) wa mwaka wa fedha.
Alisema robo ya kwanza ya mwaka huu wa fedha uchumi ulikua kwa asilimia 7; robo ya pili asilimia 7.1; ya tatu asilimia 6.2 na kwamba robo ya mwisho unatarajiwa kushuka zaidi kutokana na athari za mgawo wa umeme.
Tangu kuanza kwa mwaka huu umeme umekuwa wa mgawo, hali ambayo inaathiri uzalishaji katika sekta ya viwanda na hata utoaji huduma.
Makampuni mengi yanelazimika kutumia majenereta yanayotumia dizeli kuendelea na uzalishaji, hali ambayo inaongeza gharama za uzalishaji lakini pia kuongeza mahitaji ya dola za Marekani katika kuagiza mafuta nje.
0 Comments