Bendi ya African Stars maarufu kama Twanga Pepeta, itawatambulisha wanamuziki wake wapya kwenye onyesho lao litakalofanyika Siku ya Wapendanao kwenye ukumbi wa Da’ West Park, Tabata.
Onyesho hilo ambalo limeandaliwa na Bob Entertainment na kudhaniniwa na Dodoma Wine na Freditto Entertainment litajulikana kama Dodoma Wine Valentine Show.
Mkurugenzi wa bendi hiyo, Asha Baraka, alisema jana kuwa siku hiyo ya Februari 14 ambayo huadhimishwa na wapendanao duniani kote, watatumia kutambulisha wanamuziki wapya waliojiunga na bendi hiyo hivi karibuni wakiwemo wanenguaji.
Hata hivyo, Asha hakuwataja wanamuziki wala wanenguaji hao, lakini amesema kuwa wanatoka kwenye bendi mbalimbali maarufu nchini.
African Stars Entertainmernt (ASET) ni taasisi ya muziki ambayo kazi yake ni kuandaa na kukuza wanamuziki. Ninawaomba wapenzi wajitokeze kwa wingi siku hiyo ili waone silaha zetu mpya pamoja na rap zetu mpya,” alisema Asha.
Asha alisema pia wanamuziki wake wamejiandaa vya kutosha kuburudisha mashabiki wao siku hiyo.
Bendi hiyo inaundwa na wanamuziki machachari kama akina Charles Baba, Dogo Rama, Msafiri Diouf, Amigolas, Vena, Saleh Kupaza, Luiza Mbutu, Khadija Mnoga ‘Kimobiteli’ na Janet Isinika katika safu ya uimbaji.
Katika safu ya upigaji vyombo wapo
Jojo Jumanne, Adolph Mbinga, Thabiti Abdul, Miraji Shakashia, Gody Kanuti, Kado, Victor Mkambi, Haji wa BSS, James Kibosho, MCD na wengineo
Kwa wanenguaji wapo Super K, Saidi, Mandela, Abdilahi Zungu, Asha Sharapova, Lilian Internet, Aisha Madinda, Maria Soloma, Vicky na Regina.
Kwa upande wake Charles Baba amesema wamejiandaa vya kutosha kuwapa burudani wapenzi wao burudani ya kiwango cha juu.
Naye mratibu wa onyesho hilo Joseph Kapinga, amesema kutakuwa na zawadi mbalimbali itakayotolewa kwa maashabiki wa bendi hiyo inayotamba na staili ya `Kisigino.’
Nyimbo zilizomo kwenye albamu hiyo ni pamoja na wimbo waliorekodi na mwanamuziki nyota kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Bozi Boziana .
Nyingine zinazotamba ni ‘Mwana Dar es Salaam’, ‘Shida ni Darasa’, ‘Rafiki Adui’, ‘Mwisho wa Ubaya ni Aibu’, ‘Nazi Haivunji Jiwe’ na ‘Sitaki Tena’.