Mkutano wa pili wa Bunge la 10 ulioanza kwa kikao chake cha kwanza jana, ulichemka na kuongeza hali ya kuhasimiana miongoni mwa wabunge.
Ikiwa ni siku yake ya kwanza tu, mgawanyiko wa wazi na wenye hisia kali miongoni mwa wabunge ulijionyesha waziwazi safari hii si baina ya wabunge wa kambi ya upinzani na wale wa chama tawala, CCM tu, bali pia miongoni mwa wabunge wa kambi hiyo.
Uhasama huo umechochewa na mapendekezo ya kubadili kanuni za Bunge ili kuruhusu kuundwa kwa kambi moja ya upinzani itakayoshirikisha vyama vyote vya upinzani, hoja ambayo inasukumwa kwa kupitia vyama vya upinzani vyenye wabunge wachache, lakini wakisaidiwa na wale wa CCM.
Katika mjadala huo, wabunge kutoka CCR-Mageuzi, UDP na CUF kwa kusaidiwa na wa CCM walilumbana na wabunge wa Chadema, hali ambayo ilimpa wakati mgumu Spika wa Bunge, Anne Makinda, katika kudhibiti hisia za baadhi wabunge waliokuwa wanataka maelekezo ya kiti na wengine wakitoa taarifa.
Mjadala huo ulisababisha wabunge hao kutoleana lugha kali yakiwemo matusi na kumlazimisha Spika Makinda, kusimama kila wakati kuingilia kwa kutoa maelezo ya ziada ama kusikiliza wabunge wengine walikuwa wanaomba mwongzo wa Spika.
HOJA ZA MABADILIKO
Kabla ya mjadala huo kuanza, Naibu Spika, Job Ndugai, aliwasilisha bungeni hoja ya kufanya mabadiliko katika kanuni za kudumu za Bunge, toleo la mwaka 2007 chini ya kanuni ya 152 (2).
Mheshimiwa Spika alipokea barua ikiwa imewekwa saini na wabunge wawili, Mhe. Hamad Rashid Mohamed (CUF) na David Kafulila (NCCR-Mageuzi), wakiomba kwamba, Kanuni ya 113 (11) ya kanuni za Kudumu za Bunge, toleo la 2007 ifanyiwe marekebisho,” alisema Ngugai.
Alisema sababu ya wabunge hao kuomba marekebisho ya kanuni hiyo ni kwamba, kwa maoni yao, neno “Rasmi” lililopo kwenye kanuni hiyo linaiweka nafasi ya uenyekiti wa kamati zinazosimamia matumizi ya fedha za umma chini ya Chama kimoja cha Upinzani cha Chadema; kitu ambacho kinavinyima vyama vingine vya Upinzani vinavyowakilishwa bungeni fursa ya kuongoza kamati hizo.
Ndugai alisema aidha, wabunge hao waliomba neno “Rasmi” lifutwe katika kanuni hiyo ili kutoa haki na fursa kwa Mbunge yeyote anayetoka katika chama chochote cha Upinzani kinachowakilishwa bungeni kugombea na kuchaguliwa kuongoza kamati zinazosimamia matumizi ya fedha za umma.
Hamad na Kafulila kwa mujibu wa Ndugai, walihitimisha katika barua yao ya ombi lao kwa Spika kwa kuomba marekebisho yaliyopendekezwa yafanyike kabla ya kuundwa kwa Kamati za Kudumu za Bunge.
Kwa kuwa suala lenyewe ni la kikanuni; na kwa kuwa, kwa mujibu wa Kifungu cha 3 (3) (b) cha nyongeza ya nane ya kanuni za Kudumu za Bunge, toleo la 2007, suala lolote la kikanuni linapaswa kushughulikiwa na Kamati ya Kanuni, ni dhahiri kwamba suala hili lingeliweza kushughulikiwa iwapo Kamati ya kanuni za Bunge haingeundwa,” alisema Ndugai katika hoja yake.
Alisema kwa kuzingatia hali hiyo, busara za Spika zilitumika katika kulifanyia kazi suala hilo kwa kufanya uamuzi ufuatao:-
Kwamba, kwa kuwa suala husika ni la kikanuni na linapaswa kushughulikiwa na Kamati ya kanuni za Bunge, ni lazima Kamati hiyo iundwe kwanza kabla ya Kamati nyingine za kudumu za Bunge kuundwa ili ilifanyie kazi suala lenyewe;
Kwamba, baada ya kuundwa, kamati ya kanuni za Bunge, kwa mamlaka iliyonayo kwa mujibu wa Kifungu cha (3) (3) (a) na (b) cha nyongeza ya nane ya Kanuni za Kudumu za Bunge, toleo la 2007, lifanyie kazi pendekezo hilo na suala la Uundaji wa kanuni za Kudumu za Bunge na kutoa mapendekezo yake bungeni kwa mujibu wa masharti ya kanuni ya 152 (1) ya kanuni za Bunge.
Kwamba, ili kuondoa utata wa tafsiri, kamati ya kanuni za Bunge ijadili na kupendekeza tafsiri iliyo wazi ya maneno”Kambi Rasmi ya upinzani Bungeni”;
Kwamba, ili kuwezesha mchakato wa uundwaji Kamati za Kudumu za Bunge, Kamati ya kanuni za Bunge ishughulikie pia mapendekezo ya mabadiliko ya majina ya Kamati hizo ili yaendane na Muundo wa sasa wa wizara za Serikali;
Kwamba, kwa ajili ya uendeshaji bora wa shughuli za Bunge, Azimio la kufanya mabadiliko ya kanuni husika na pia pendekezo la kutengua Kanuni ya 153 (1) yawasilishwe bungeni na Naibu Spika katika mkutano huu wa Pili wa Bunge, ili kuwezesha mchakato wa kuunda Kamati za Kudumu za Bunge kukamilika haraka iwezekanavyo.
Ndugai alisema katika kutekeleza uamuzi wake, Spika aliunda na kuteua wajumbe wa Kamati ya Kanuni za Bunge kwa kuzingatia masharti yta Kanuni ya 113 (4), pamoja na Kifungu cha 3 (1) cha Nyongeza ya nane ya Kanuni za Bunge ili kufanyia kazi suala hilo.
Wajumbe walioteuliwa kuunda Kamati hiyo ni Anne Makinda, Job Ndugai, William Lukuvi, Freeman Mbowe, Jaji Frederick Werema, Anna Abdallah, Mustapha Akunaay, Tundu Lissu na Andrew Chenge.
Wengine ni Felix Mkosamali, Angela Kairuki, Mohamed Mnyaa, Hamad Rashid Mohamed, George Simbachawene, Pindi Chana na Nimrod Mkono.
Kwa mujibu wa Ndugai, kifungu cha 3(3) cha nyongeza ya nane ya kanuni za kudumu za Bunge toleo la 2007, pamoja na mambo mengine, kinaeleza kwamba, moja ya majukumu ya Kamati ya Kanuni za Bunge ni:-
Moja, Kujadili na kutoa mapendekezo juu ya kufanya mabadiliko katika Kanuni za Bunge; na mbili, kuchunguza na kutoa taarifa juu ya pendekezo lolote linalohusu kanuni za kudumu za Bunge ambalo limepelekwa kwa kamati hiyo ya Spika au Mbunge yeyote.
Kwa mamlaka iliyopewa kwa iliyopewa kwa mujibu wa vifungu hivyo kamati ya Kanuni za Bunge ilikutana Jumatatu Februari 7, mwaka huu na mara baada ya kikao cha kupeana taarifa kujadili mapendekezo ya marekebisho ya Kanuni za Kudumu za Bunge.
Katika kushughulikia mapendekezo hayo, kamati hiyo ilijadili na kupitia kwa makini Kanuni za Bunge zinazohusika ili kubaini kama ni kweli au la “Kambi “Rasmi” ya upinzani Bungeni,” inaundwa na chama chenye haki ya kuchagua kiongzi wa kambi rasmi ya upinzani Bungeni, kama inavyodaiwa na wabunge waliowasilisha maombi ya Marekebisho ya Kanuni.
Kutafsiri maneno “Kambi Rasmi ya upinzani Bunni”.
Kanuni ya 14 hadi ya 16 zinafafanua kuhusu kiongozi wa kambi Rasmi wa Upinzani Bungeni na jinsi anavyochaguliwa.
Kanuni hizo pia zinafafanua chama chenye haki ya kumchagua Kiongzi wa kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ni kile chenye idadi kubwa yta wabunge wasiopungua asilimia 12.5 ya wabunge wote.
Aidha, kanuni 15(2) inafafanua pia kuwa Kingozi wa “Kambi rasmi ya upinzani Bungeni atateua wabunge wa chama chake au wabunge wa kambi rasmi ya upinzani Bungeni” ambao watakuwa wasemaji wakuu wa kambi ya upinzani kwa wizara zilizop za serikali.
Ndugai alisema kutokana na masharti ya kanuni hiyo, Kamati ya kanuni za Bunge iliridhika pasipo mashaka yoyote kwamba, tafsiri sahihi ya maneno “Kambi Rasmi ya uapinzani Bungeni” ni kambi inayundwa na vyama vya upinzani vinavywasilishwa bungeni kwa mujibu wa masharti ya fasihi ya (2) ya kanuni za Kudumu za Bunge.
Alieza kuwa kwa tafsiri hiyo si kweli kwamba “Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni” inaundwa na chenye wabunge wengi na chenye haki ya kuchagua kingozi wa kambi rasmi ya upinzani Bungeni.
Ndugai alisema kwa kuzingatia ukweli huo, Kamati ya kanuni za Bunge ilipendekeza kwamba maneno “Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni” yawekewe tafsiri ifuatayo:-
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni” maana yake ni kambi ya upinzani iliyoundwa na vyama vya upinzani vinavyiwakilishwa bungeni kwa mujibu wa masharti ya fasihi (2) ya kanuni ya 14 ya kanuni hizi”.
Alisema kuwa kamati hiyo ilijiridhisha pia kwamba tafsiri hiyo itaondoa utata uliopo na kulifanya ombi la wabunge wahusika la kuifanyia marekebisho kanuni ya 113 (11) kutokuwa na ulazima wowote.
Kwa hali hiyo, Kamati ya Kanuni za Bunge imetoa mapendekezo ili yaridhiwe na Bunge kwa mujibu wa Kanuni ya 152 (2).
Baada ya Ndugai kuwasilisha hoja hiyo, wabunge kadhaa walipata nafasi ya kuchangia na ndipo malumbano yalipoanza.
KAFULILA
David Kafulila (Kigoma Kusini-NCCR-Mageuzi), alipongeza maamuzi yaliyofikiwa na kamati ya Kanuni za Bunge kwa kutaka kuundwa kwa kambi moja ya wapinzani na kueleza kuwa ilikuwa ni aibu kwa kambi moja kuhitilafiana.
Kafulila alisema walikuwa wanakataa marekebisho ya kanuni hawakuwa na hoja za msingi, bali ulikuwa ni ubaguzi na kuongeza kuwa sasa kutakuwa na haki na usawa katika kambi ya upinzani.
Aliahidi kuwa wabunge wa chama chake watakuwa waaminifu na watiifu kwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni.
HAMAD RASHID MOHAMED
Hamad Rashid Mohamed (Wawi-CUF), alisema kuwa Bunge la Tisa halikuweka tafsiri nzuri kuhusu kanuni za Bunge.
Hata hivyo, aliilaumu Chadema kwa kushikilia msimamo wa kukataa kubadili kanuni za Bunge wakati CUF kilipokuwa kikiongoza upinzani Bungeni baadhi ya viongozi wengine wa kambi ya upinzani walipewa fursa ya kugombea na kuongoza kamati za fedha za umma.
Alitoa mfano kwa Dk. Willbroad Slaa, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa, Zitto Kabwe aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma na Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali, John Cheyo.
Alisema pamoja na kwamba Chadema inajifanya kuwa chama kikubwa kwa kuwa na wabunge wa majimbo 23, lakini CUF ina majimbo 28.
Pia alisema Zanzibar bila kujali udogo wa eneo lake ilikuwa ni nchi huru na mwanachama wa Umoja wa Mataifa na kwamba bila Zanzibar Tanzania haiwezi kuwepo.
Hata hivyo, Tindu Lissu (Chadema-Singida Mashariki), aliingilia kati na kumtaka Hamad afute kauli yake aliyoisema wakati akichangia kwamba Chadema iache mambo ya kitoto.
Lissu pia alimtaka Spika amzuie Hamad kuzungumzia mambo ya Muungano kwa sababu hayakuwa ndani hoja iliyokuwa inajadiliwa.
HALIMA MDEE
Alisema kuna hatari kuruhusu chama cha kimoja chenye idadi kubwa ya wabunge kuunda kambi moja ya upinzani na vyama vyenye idadi ndogo ya wabunge.
Alisema hatari inatokana na uwezekano wa baadhi ya ajenda kupelekwa bungeni zikiwa na maslahi ya watawala.
Halima ambaye uchangiaji wake ulikuwa ukisababisha wabunge kadhaa wa CCM kusimama na kuomba mwongozo wa spika, alisema tafsri ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaundwa na chama chenye wabunge wengi bungeni kwa kuwa si rahisi kiongozi wa upinzani bungeni kuwabana watu ambao hawatoki katika chama chake na kuzingatia Chadema ina wabunge zaidi ya asilimia 12.5.
Alisema: “Hii ni kufunika kombe mwanaharamu apite, sisi hatuna shida na wenyeviti wa kamati.”
JOHN CHEYO
John Cheyo (UDP-Bariadi Mashariki) alisema kimsingi Watanzania wanahitaji wabunge wengi wa upinzani wenye nguvu na kuitaka Chadema iache jazba.
Alisema wajenge Bunge litakaloleta matumaini kutoka Bungeni.
GEORGE SIMBACHAWENE
George Simbachawene (CCM- Kibakwe) alisema anashangaa kwa nini Chadema inavibagua vyama vingine vya upinzani na kuvinyima haki ya kuchagua na kuchaguliwa.
TUNDU LISSU
Tundu Lissu alisema barua za Kafulila na Rashid, zilionyesha kuwa walitaka vyama vyao viruhusiwe kugogombea uongozi wa kamati za fedha za umma wakati Watanzania hawakuvipa ridhaa ya kuwa na wabunge wengi bungeni.
Alisema kwamba utamaduni, mila na desturi ya mabunge ya Jumuiya ya Madola ambayo Tanzania imekuwa ikifuata, kambi ya upinzani imekuwa ikundwa na chama chenye wabunge wengi bungeni na zile kamati za fedha za umma huongozwa na chama hicho hicho.
Alisema kama kamati hizo zitapewa vyama vyenye wabunge wachache huku mbele kashfa za Dowans, Richmond na Epa Watanzania hawatazisikia zikifichuliwa.
Alisema chama kama CUF kimeshapata Makamu wa Kwanza wa Rais baada ya kuundua serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar, hali ambayo imeua kambi ya upinzani Zanzibar.
Alisema sio ndoa ya mapenzi bali ni ndoa ya kulazimisha ambayo inaruhusu wake wengi, lakini hairuhusu waume wengi.
KHALIFA SULEIMAN KHALIFA
Khalifa Suleiman Khalifa (CUF-Gando), alisema mjadala huo umempa picha ya dharau dhidi ya wabunge wa Zanzibar na kwamba nongwa ni uongozi wa kamati za Bunge.
CHADEMA WATOKA BUNGENI
Akichangia mjadala huo, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe, ambaye alikuwa wa mwisho kuzungumza baada ya Mbunge wa Ubungo, kutoa taarifa utaratibu kwamba ni utamaduni na kanuni hoja za kiserikali kupewa fursa kiongozi wa upinzani kueleza maoni yake, alieleza masikitiko yake juu ya hoja hiyo ilivypenyezwa bungeni.
Mbowe alisema Chadema wana tofauti za kimsingi na CUF ambao ni sehemu ya serikali iliyoko madarakani, na kwamba hawakubaliani na ushirika wa kulazimishwa.
Mbowe alisema lengo la mabadiliko hayo ni kama kuwachagulia washirika wa kuunda kambi ya upinzani bungeni. Alisema wananchi ndio walioamu kuipa Chadema fursa ya kuwa chama cha pili bungeni baada ya kuipa kura nyingi katika uchaguzi mkuu uliopita.
Alilaumu CCM kutumia wingi wao kupotosha ukweli wa hoja hiyo na kusema kuwa hatua hiyo siyo ya kujenga bali ni ya kubomoa.
Alisema yeye ataongoza kambi ya Chadema na ndio msimamo wake na dhamira ya chama chake kwamba asipofanya hivyo atakuwa anawanyima haki Watanzania milioni 2.8 waliowachagua.
Baada ya mchango huo, Mbowe alimuomba radhi Spika kwamba wao kama kambi ya upinzani hawatakuwa sehemu ya mwisho ya mjadala huo, kwa maana ya kupitisha azimio la kutenguliwa kwa kanuni hiyo.
Kwa kauli hiyo, wabunge wote wa Chadema walitoka nje ya ukumbi wa Bunge na kuwaacha wabunge wa CCM, CUF, NCCR-Mageuzi, TLP na UDP, ambao walipitisha kanuni hiyo.
Wakati wakitoka, baadhi ya wabunge wa CCM walipiga vijembe wengine wakisema: “Tumeshawazoa hao, waroho wa madaraka, mtarudi tena na posho msichukue.”
Naye Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Stella Manyanya, alisimama na kutaka mwongozo wa Spika kuhusiana wabunge wa chama hichokutoka nje bila kuzingatia taratibu wa kusalimu kiti ama kwa kuinamisha kichwa au kupiga koti.
Hata hivyo, Spika Makinda alisimama na kusema kuwa alimuona kiongozi wa upinzani (Mbowe) akiinamisha kichwa chini wakati wakitoa hoja ya kutokuunga mkono hatua ya mwisho kupitisha kanuni hiyo.