Wafanyabiashara ndogondogo mjini hapa maarufu kama machinga, wamepambana vikali na askari polisi katika purukushani ambazo askari mmoja ameporwa bunduki aina ya SMG aliyokuwa nayo.
Mapambano hayo yalianza baada ya askari hao kuanza zoezi la kuwapora wamachinga hao bidhaa zao kwa madai kuwa wanafanya biashara katika eneo lisiloruhusiwa na Manispaa.
Askari hao wakiwa pamoja na wafanyakazi wa Manispaa, walivamia eneo hilo na kuanza kuwakimbiza wafanyabiashara katika eneo hilo na kuwapora bidhaa walizokuwa wanaziuza.
Wakati askari wakiendelea na zoezi hilo, wamachinga hao walianza kuwarushia mawe hali iliyosababisha baadhi ya wafanyakazi wa Manispaa walioambatana na askari hao kukimbia.
Baada ya wafanyakazi hao kukimbia pamoja na mgambo wao, askari wawili walibaki eneo hilo wakiwa na silaha.
Wamachinga hao walifanikiwa kumpora askari mmoja silaha yake hali ambayo ilimlazimu mwenzie kutaka kutumia aliyobaki nayo kuwapiga waliokuwa wana mzonga.
“Yaani leo ingekuwa hadithi nyingine tena kwani wakati yule askari ameporwa silaha mwenzake alishaikoki akitaka kuanza kuitumia, lakini bahati nzuri Mheshimiwa Mbunge wa Maswa Mashariki (Chadema), John Shibuda, alikuwa benki akatoka na kuja kutuliza vurugu za wafanyabiashara na askari,” alisema Alela Abdul, mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo.
Shibuda aliwasihi wamachinga hao kuacha tabia ya kupokonya askari silaha kwani ni hatari kwao.
“Mnaweza kumpora askari silaha na mwenzake akaitumia ile nyingine kupambana na ninyi kwa kudai ni majambazi …kama kuna tatizo jitahidini kutafuta njia nyingine ambazo ni nzuri, lakini sio kupora askari silaha,” alisema Shibuda.
Baada ya hali ya hewa kutulia eneo hilo wafanyabiashara hao walirejesha kwa askari huyo bunduki waliyopora na kuanzia hapo hali ya amani ikawa ya kawaida.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma, Suzan Bidya, alisema hata kama wamachinga hao watawapiga askari hao, lakini zoezi la kuwatoa katika eneo hilo litaendelea kwa kuwa haliruhusiwi kufanya biashara.
“Lile eneo ni maalum kwa watembea kwa miguu pamoja na maduka yaliyopo eneo hilo, lakini kama wao wataendelea kubaki hapo kila siku watakutana na askari,” alisema Bidya.
0 Comments