POLISI wamemkamata mkazi wa Kijiji cha Mwamala wilayani Nzega katika mkoa wa Tabora, Tano Katinda, akiwa katika harakati za kuuza kichwa cha mtu anayesadikiwa kuwa ni mkewe na viungo vingine vya mwili wa mwanamke.
Katinda alikamatwa Ijumaa asubuhi wakati alipokwenda kuuza 'bidhaa' hizo kwa Polisi waliokuwa lindoni benki.
Mtuhumiwa huyo pia amekutwa na sehemu nyingine za viungo vya mwili yakiwemo matiti na sehemu za siri za kike.
Alikuwa akizunguka na viungo hivyo vikiwa katika mfuko wa plastiki maarufu kama Rambo kwa lengo la kusaka wateja katika mitaa ya mjini wa Kahama mkoani Shinyanga.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Diwani Athumani, amethibitisha kukamatwa kwa mwananchi huyo, na kwamba, mtuhumiwa alikamatwa jana saa 3 asubuhi baada ya kufika katika benki ya CRDB, tawi la Kahama.
Alisema , baada ya kuzunguka kutafuta soko la viungo hivyo vya binadamu hadi katika Stendi Kuu ya mjini Kahama, akidai anauza nyama ya nguruwe maarufu kama Kitimoto, baadhi ya watu walimwelekeza akawauzie watu waliopo eneo na benki.
Katinda alisonga mbele hadi tawi la NMB akawakuta askari aliowatangazia kuwa anauza kitimoto, walimjibu kuwa wao ni Waislamu, labda akajaribu kwa askari waliokuwa lindo katika benki ya CRDB iliyopo jirani na NMB.
Anasema, mtuhumiwa alitii ushauri huo na kusonga mbele hadi CRDB alikoinadi nyama aliyokuwa anaiuza.
Lakini mmoja wa askari hao baada ya kuchungulia alibaini kuna kichwa cha binadamu na viungo vingine, walimweka chini ya ulinzi na kumfikisha katika kituo cha polisi cha wilaya, mjini Kahama.
“Awali kijana huyo alionekana kwenye eneo la stendi mabasi maeneo ya CCM Kahama akiuza viungo, hivyo ndipo alipoelekezwa kwenda kuuza kwa askari waliokuwa katika malindo ya benki za CRDB na NMB huku watu hao wasijue kijana huyo ni nini amebeka katika furushi lake,” alisema Kamanda Athumani.
Kwa mujibu wa kamanda huyo wa polisi, kijana huyo baada ya kukamatwa alikiri kuwa viungo hivyo vilikuwa vya mke wake aliyetajwa kwa jina la Kabula Luziga (18), mkazi wa Itobo, Nzega.
Alisema, kijana huyo baada ya kuulizwa alisema alimuua mkewe usiku kwa kutumia panga baada ya kumvizia akiwa amelala.
Mtuhumiwa huyo aliwaeleza Polisi kuwa, kiwiliwili cha mwili wa marehemu Luziga alikiacha katika chumba chake nyumbani kwa babu yake aliyemtaja kwa jina moja la Mwanandilila huko katika Kijiji cha Mwamala, Nzega.
Hata hivyo, kamanda huyo alisema baada ya kumhoji kijana huyo alidai kuwa alisikia matangazo kwenye kituo kimoja cha Redio cha mjini Kahama kuwa, viungo hivyo ni mali na tayari kuna wateja wanaovihitajika, ndipo alipoamua kumuua mkewe
ingawa wakati akiuza alidai ni nyama ya kitimoto.
Kamanda Athumani amesema, jeshi la Polisi linaendelea na upelelezi ikiwa ni pamoja na kuchunguza akili ya kijana huyo.
Kikosi cha askari polisi mjini hapa kiliondoka jana mchana kwenda kijijini Mwamala kuona kama kweli kuna kiwiliwili cha marehemu Luziga.
0 Comments