Walioshuhudia wamesema waasi wa Libya wanakaribia kupambana na majeshi yanayomtii Kanali Gaddafi kwenye mji wa Ajdabiya.
Ndege za Ufaransa na Uingereza zimerusha mabomu karibu na mji ulio mashariki mwa nchi hiyo wakati wa usiku, yakiwemo makombora ya serikali.
Waasi walijaribu kuwashambulia wanajeshi wanaomwuunga mkono Gaddafi baada ya kufanyika mashambulio ya ndege, lakini walisema ilibidi waghairi.
Mji huo umezingirwa kwa siku kadhaa sasa. Wakazi waliokimbia walisema mitaa ilibaki mitupu, na majeshi ya serikali yalikuwa yakifyatua risasi kiholela.
Majeshi ya nchi za magharibi yalianza kushambulia kwa mabomu wiki iliyopita kwa nia ya kutekeleza azimio la Umoja wa Mataifa lililozuia majeshi ya Libya kuwashambulia raia kwa ndege.
Majeshi ya umoja wa nchi za kujihami za Ulaya, Nato yanatarajiwa kuongoza harakati hizo za kijeshi badala ya Marekani kwa siku zijazo.
Maafisa wamesema uvamizi huo umedhoofisha majeshi yanayomwuunga mkono Gaddafi kwa kiwango kikubwa, lakini mapigano yameendelea Misrata kwa upande wa magharibi na Adjabiya huko mashariki.
0 Comments