Hakimu Mkazi, Aloyce Katemana, aliyekuwa anayesikiliza kesi ya madai ya Shilingi Milioni Mia Moja kwa kuitwa fisadi papa, iliyofunguliwa na mfanyabiashara, Yusuf Manji, dhidi ya Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Reginald Mengi, amejitoa kuisikiliza kesi hiyo.
Hata hivyo, Hakimu Katemana, ambaye alitangaza kujitoa kusikiliza kesi hiyo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, hakuweka bayana sababu za kufanya hivyo.
"Kesi hii imepangwa kutajwa leo (jana), lakini najitoa kuisikiliza sababu za kujitoa kwangu sitazisema hadharani narejesha jalada kwa Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hii ili aipangie hakimu mwingine," alisema.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Aprili 15, mwaka huu itakapotajwa tena.

Awali, Manji alidai Aprili 23-27 mwaka 2009, Mengi kwa kutumia kituo cha Televisheni cha ITV, alitoa madai kuwa Manji na wafanyabiashara wengine kuwa ni mafisadi papa, wanahamisha rasilimali za taifa kupeleka nje ya nchi na kwamba wameshiriki kikamilifu katika ufisadi wa ununuzi wa magari ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), rada, mradi wa makaa ya mawe wa Mchuchuma, mifuko ya hifadhi ya jamii ya PSPF na NSSF, Dowans na Richmond.