Vigogo wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), mkoani Mbeya, wamekihama chama hicho na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Vigogo hao ni Mwenyekiti wa Chadema mkoani Mbeya, Sambweli Shitambala na Katibu Mwenezi wa chama hicho wilayani  Ileje, Henry Kayuni.
Wote wawili walipokewa na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete mjini hapa jana.
Akizungumza wakati wa hafla ya mapokezi hayo, Shitambala alisema amejiunga na CCM kwa ridhaa yake.
Aidha, alisema anamheshimu Rais na anasikitishwa na baadhi ya wenzake wanaofanya tofauti na hivyo.
Unajua mtoto aliyelelewa vyema huwa hatukani wazazi wake, si mbishi…kama kuna kitu anataka kumshauri baba yake, haanzi kwa kumtukana kwani atamuona hopeless (hafai),” alisema.
Kwa upande wake, Kayuni alisema ameamua kukihama Chadema kutokana na kuchoshwa na ahadi hewa ambazo zimemsababishia kuingia kwenye madeni makubwa.
Alisema aligombea ubunge Jimbo la Ileje kwa tiketi ya Chadema lakini fedha zote alizimaliza katika kipindi cha uchaguzi kwa kudanganywa kwamba atakuwa akipatiwa ruzuku, jambo alilodai kuwa si la kweli.
Akiwapokea viongozi hao kutoka kambi ya upinzani, Rais Kikwete alisema kutakuwepo na vyama vingi vya siasa nchini lakini chama pekee ni CCM na vingine ni vya wanaharakati.
Alisema kwa sasa wasahau yaliyopita na wagange yaliyopo na yajayo ili kukijenga chama.
Walitambulishwa mbele ya viongozi na wanachama wa CCM na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho mkoani Mbeya, Profesa Mark Mwandosya.
Profesa Mwandosya pia alisema wanatarajia kuwapokea wanachama wengine 150 kutoka Chadema.