Hatimaye hali ya mwanamuziki mkongwe wa muziki wa dansi nchini, Muhidini Maalim Gurumo (68) imeanza kuimarika baada ya kupata fahamu.
Gurumo ambaye amelazwa katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam juzi akiwa katika hali mbaya, anapatiwa matibabu matatizo ya moyo, ugonjwa unaomsumbua kwa miaka mingi na kupelekea mwaka jana kulazwa hospitalini hapo.

Afisa Uhusiano Msaidizi wa Muhimbili, Jezza Waziri alieleza hali ya mwanamuziki huyo ambaye pia ni kiongozi wa bendi ya Msondo Ngoma, imeanza kuimarika ambapo jana alirejewa na fahamu pamoja na kuweza kuongea japo kwa taabu.
"Tungependa kueleza kwamba Mzee Gurumo ameanza kupata nafuu, hivi sasa ameanza kupata fahamu na kurejewa na kumbukumbu kidogo kuliko hali aliyokuja nayo jana ambayo ilikuwa mbaya," alisema waziri.
Alisema mwanamuziki huyo amelazwa wodi namba moja Jengo la Mwaisela lakini kutokana na ushauri wa madaktari watu hawaruhusiwi kumuona ili kumfanya aweze kupumzika.
"Pamoja na kupata unafuu hatutaweza kuwaruhusu watu kumuona kwa sasa kutokana na ushauri wa madaktari ila akiendelea kupona tutatoa maelekezo mengine," aliongeza.
Gurumo anayejulikana na wapenzi wengi wa muziki kutokana na kuwa na kipaji kikubwa cha kuimba na kutunga nyimbo, alifikishwa hapo juzi majira ya saa 2:30 asubuhi kwa ajili ya kupatiwa matibabu baada ya hali kuwa mbaya.
CHANZO: NIPASHE