Upepo unazidi kugeuka kwa wakazi wa Gongo la Mboto ambao nyumba zao zilipata madhara ya milipuko ya mabomu, na sasa imethibitishwa kwamba ni nyumba 73 tu ndizo zitajengwa upya.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki, alitoa ripoti hiyo jana mbele ya makatibu wakuu kutoka wizara tofauti za serikali waliofika eneo hilo kwa ajili ya kutoa msaada wao binafsi wa Shilingi milioni sita kwa waathirika hao.
Msaada huo ulikabidhiwa na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma), George Yambesi, kwa niaba ya Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo.

Sadiki aliwaambia makatibu hao kuwa kati ya nyumba 73 zitakazojengwa upya, nyumba 26 wamiliki wake watajengewa nyumba maeneo mengine kutokana na nyumba zao zilizoharibika kujengwa mabondeni ambako ni sehemu hatari.
“Wamiliki hawa baadhi watajengewa nyumba mpya maeneo ya Kinyerezi, Geza Ulole na mmoja yupo Kinondoni ambaye atajengewa huko, tutatumia Sh. milioni 96 kwa ajili ya fidia na mambo mengine kwenye nyumba hizi,” alisema.

Alisema nyumba nyingine 1,693 ambazo zilipata uharibifu kidogo zitakarabatiwa.
Alisema ujenzi wa nyumba hizo unatarajia kuanza wakati wowote kuanzia sasa.
Alisema tayari wamekwisha kuikabidhi Suma-JKT Sh. milioni 30 kwa ajili ya ununuzi wa saruji ili kufyatua

matofali na usagaji wa kokoto.
“Suma-JKT imeshaanza zoezi la ufyatuaji matofali, tunatazamia ujenzi huu utaanza wakati wowote kuanzia sasa,” alisema.
Alisema tenda ya utengenezaji wa mandhari ya nyumba hizo ilikabidhiwa kwa wataalam wa Chuo Kikuu cha Ardhi, ambao wameshakamilisha uchoraji wake na kwamba wameshakamilisha kazi ya uchoraji na wanachokifanya hivi sasa ni kuziingiza kwenye mashine maalum ili kuwakabidhi. Alisema mara baada ya kazi hiyo kukamilika, ujenzi wa nyumba utaanza. “Tutatoa upendeleo kidogo kwa zile nyumba ambazo kabla ya athari hizi kutokea vyumba vyake vilikuwa vidogo sana hivyo vitapanuliwa ili nao waishi kwenye mazingira mazuri,” alisema.
Kadhalika, alisema kazi ya ulipaji wa mirathi limeshaanza na tayari wameshawalipa watu wawili kiasi cha Sh. milioni 17. Alisema fedha za kuwalipa watu mirathi zipo tayari wanachosubiri ni wahusika wakamilishe taratibu za kisheria.
Sadiki aliwaomba wale wote wanaoshi kwenye mahema ambayo wakati wa mvua huvuja watoe taarifa ili wabadilishiwe kwa sababu bado yapo mengine.

MISAADA ZAIDI YAMWAGWA
Wengine waliotoa misaada ni pamoja na waumini wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam wakiongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo hilo, Mwadhama Policarp Kardinali Pengo ambao walikabidhi msaada wa Sh. milioni 25.
Akikabidhi msaada huo kwa niaba ya Kardinali Pengo, Askofu Msadizi jimbo hilo, Selutaris Libena, alisema msaada huo wa vyakula, nguo, fedha na vifaa vingine umetokana na misa takatifu iliyofanyika Kanisa la Pugu Machi 12, mwaka huu kwa ajili ya kuwaombea waathirika hao.
Alisema msaada wa vyakula walivyovikabidhi ni pamoja na unga wa sembe kilo 930, mchele kilo 400, sukari kilo 82, chumvi katoni mbili, mafuta ya kupikia lita 42, majani ya chai katoni moja na maharagwe kilo 129 vyenye thamani ya Sh. milioni 2.
Vitu vingine ni sabuni za vipande katoni 57, viatu viroba vitano na viberiti katoni tatu vyenye thamani ya Sh. 800,000.
Askofu Libena alisema msaada wa nguo una thamani ya Sh. milioni 2.5 na kwamba walitoa hundi ya Sh. milioni 19.8 .
Alisema thamani ya vitu vyote pamoja na fedha hizo ni zaidi ya Sh. milioni 25.
Nayo, Benki ya Biashara ya Kenya (KCB), ilitoa msaada wa vitu vyenye thamani ya Sh. 2,000,000.
Akikabidhi msaada huo, Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Joram Kiarie, alisema msaada huo ni sehemu ya programu za KCB za kuchangia sekta mbalimbali za elimu na afya kila mwaka.
Nao Umoja wa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa Wilaya ya Kinondoni ulikabidhi katoni kumi za maji pamoja na fedha taslimu Sh. 600,000 wakati Idara ya Jinsia na Wanawake na Walemavu kutoka Chama cha Walimu Tanzania (CWT) ilikabidhi fedha taslimu Sh. milioni 1.5.
Akishukuru kwa niaba ya serikali, Sadiki aliziomba taasisi, mashirika makampuni na watu binafsi wajitokeze kuwasaidia wenzao kwa sababu misaada bado inahitajika wakati kazi ya kuwajengea nyumba ikitazamiwa kuanza wakati wowote.