Aliyekuwa mwanachama maarufu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Abdalah Safari, amejiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kukimwagia sifa kuwa hakina udini wala ubaguzi.
Alisema safari yake ya kujiunga na chama hicho imechukua muda wa miezi mitatu ya majadiliano kwa kuwa baada ya kutoka CUF ambako alipata misukosuko mingi, familia yake ilimshauri apumzike.
“Baada ya misukosuko ya CUF familia yangu iliogopa sana mimi kurudi tena kwenye siasa, mke wangu na watoto walinishauri nitulie na niendelee na kufanyakazi ya kutunga vitabu tu, mke wangu hakutaka kabisa nirudi kwenye siasa, lakini nimekaa nao na tumefikia mwafaka ndo maana leo hii niko Chadema,” alisema jana.

Profesa Safari alitambulishwa kwa waandishi na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa, katika ofisi za makao makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam.
Alisema alifuatwa na vyama vingi vya siasa vikitaka ajiunge navyo, lakini baada ya majadiliano ya muda mrefu na viongozi wa Chadema ameona busara ni kujiunga na chama hicho na amewaomba wale wote waliokuwa wakimwuliza anakokwenda wamfuate Chadema.
Profesa Safari ambaye ni mwanasheria, alisema propaganda za kuwepo kwa udini katika Chadema zilitumiwa tu na CCM kutaka kujikusanyia kura katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana kwani yeye amechunguza na kubaini kuwa Chadema hakina udini wala ubaguzi wowote hali ambayo imemvutia kujiunga nacho.
Aidha, Profesa Safari alieleza kuwa atahamasisha nguvu ya umma itumike kuzirejesha nyumba za serikali ambazo ziliuzwa bila kufuata utaratibu.
Amemshutumu Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, kuwa hakushirikisha Bunge wakati wa kuuza nyumba hizo na badala yake alikaa kijiweni na rafiki zake na kuamua kuchukua uamuzi huo ambao alisema ulikuwa wa kihuni.
Profesa Safari alisema kwa kuwa walionunua nyumba hizo za serikali ni majaji, hata ikipelekwa kesi mahakamani kwa ajili ya kutaka kubatilisha uuzwaji wake kesi hiyo haitafika popote, hivyo njia rahisi ni kutumia nguvu ya umma kuzirejesha.
“Uuzwaji wa nyumba zile umekiuka Ibara ya 9 ya Katiba, lakini ukipeleka kesi mahakamani huwezi kushinda kwa kuwa walionunua nyumba ni hao hao watakaosimamia kesi sasa haki itapatikanaje hapo? Suluhisho hapo ni falsafa ya People’s Power (Nguvu ya Umma),” alisema. Profesa Safari pia alikumbushia vifo vya wachimbaji wadogo vinavyodaiwa kutokea katika mgodi wa Bulyanhulu mkoani Shinyanga katika miaka ya tisini na kuhoji kwanini serikali imeshindwa kukubali hata kuunda tume kuchunguza ukweli wa madai ya kufukiwa watu wakiwa hai.
“Kama habari zile hazikuwa za kweli serikali imeogopa nini kuunda hata tume ichunguze na ieleze umma kuhusu ukweli wa madai yale, hatua ya kukataa kuunda tume inaleta maswali mengi,” alisema.
Kwa upande wake, Dk. Slaa aliunga mkono kauli ya Profesa Safari ya kutaka nyumba za serikali zilizouzwa zirejeshwe kwa kuwa hakukuwa na sababu ya kufanya hivyo.
Viongozi wa Chadema walimmwagia sifa Profesa Safari kuwa ni mtu makini.
Dk. Slaa alimwelezea Profesa Safari kuwa ni mtu makini ambaye umaarufu wake unajulikana ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake, Mbowe alisema Profesa Safari ni mtu makini na mchapa kazi hivyo chama chake kitaendelea kuwakaribisha wanachama makini kwa ajili ya kuimarisha harakati za mageuzi ya kisiasa nchini.
“Hapa Chadema hatuunganishwi na dini, kabila wala sura ya mwenyekiti, kila anayejua kuwa taifa hili linahitaji tiba ya uongozi ana tiba ndani ya Chadema, akija atapokelewa,” alisema Mbowe.
Profesa Safari alijiondoa CUF mapema mwaka huu kwa madai kuwa chama hicho kimeshindwa kufikia malengo yake ya kisiasa kutokana na uongozi mbovu.
Profesa Safari aligombea nafasi ya uenyekiti wa CUF katika Uchaguzi Mkuu wa chama hicho Februari 23-27 mwaka 2008 na kushindwa na Profesa Ibrahim Lipumba.
CHANZO: NIPASHE