WANASAYANSI wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) wamesema bado wanaifanyia kazi dawa ya Mchungaji Ambilikile Mwasapila wa kijiji cha Samunge wilayani Ngorongoro, mkoani Arusha ili kubaini uwezo wa dawa yake kutibu magonjwa.
Aidha, wamesema, hivi sasa watakuwa karibu na baadhi ya watu wanaotoa tiba asilia ili kufanya nao utafiti, kwani inavyoonekana tiba asilia ni muhimu kwani inatibu magonjwa mbalimbali ya binadamu.
Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Dk. Mwele Malecela, aliyasema hayo jana mjini Arusha wakati wa ufunguzi wa Kongamano la 25 la Sayansi ya Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR).
Alisema, awali walikuwa hawatoi vipaumbele kwa watu wanaotoa tiba asilia, lakini hivi sasa kuna umuhimu wa kushirikishwa kwenye utafiti kwani baadhi ya miti shamba inatibu magonjwa ya binadamu.
Alisema, suala la tiba ya Mchungaji Mwaisapile linawaumiza vichwa wanasayansi nchini, kwani linawafanya kufikiri wafanyeje hivi sasa kwani watu wanaotoa tiba asilia wapo na baadhi yao wamesajiliwa na kuna vipengele vya sheria juu ya tiba asilia.
“Suala hili hivi sasa linaumiza vichwa vyetu, ndiyo maana tunasema tutashirikiana na watu wanaotoa tiba asilia, ili kujua magonjwa yapi yanaponeshwa kwa miti shamba pia tunafanyia kazi dawa ya Mchungaji Mwasapila, ili kujua inatibu magonjwa mangapi na tutakapokamilisha uchunguzi wetu, tutaweka bayana magonjwa yanayotibika kutokana na dawa yake," alisema Mwele.
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Haji Mponda, aliwasihi watafiti hao kutumia lugha itakayomwezesha mwananchi wa kawaida kuelewa, pia kutoa matokeo ya utafiti kwa wananchi, ili wajue magonjwa ambayo ni ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza badala ya utafiti huo kuishia kwenye makongamano pekee.
Alisema, hivi sasa pia ajali za barabarani zinazohusisha pikipiki zinaongoza kwa asilimia 38 hivyo ni bora watafiti hao kuangalia pia suala hilo na kutoa uamuzi wao kwani ndizo zinazosababisha baadhi ya watu kuwa walemavu na wengine kupoteza maisha huku wakiacha tegemezi.
Askofu Moses Kulola wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God (EAGT), amewataka baadhi ya viongozi wa dini kuacha kumhukumu Mchungaji Mwaisapile kwani atahukumiwa na Mungu ikiwa anafanya hila katika matibabu yake.
Askofu Kulola aliwaambia waandishi wa habari jana Dar es Salaam, kuwa Mchungaji huyo anayedai kutibu magonjwa sugu matano, kwa dawa aliyooteshwa na Mungu kuwa yeye anamwona kama mganga wa kienyeji anayetoa dawa, hivyo anayemwamini aende.
Alisema kinachotakiwa ni kwamba anayeona anaweza kusaidiwa naye aende, huku akiwasihi baadhi ya viongozi wa dini kutumia busara katika kumzungumzia Mchungaji huyo na kuacha tabia ya kumhukumu.
“Katika Neno la Mungu anasema acheni magugu yamee na ngano naye ndiye atayachambua siku za mwisho, hivyo kama anafanya hila katika utoaji tiba, atahukumiwa na Mungu siku za mwisho,” alisema Askofu Kulola
Aidha, aliwataka viongozi wa madhehebu mbalimbali kuacha tabia ya kusema kuwa dini moja ndiyo nzuri kuliko nyingine, suala hilo ni ubaguzi wa Neno la Mungu kwani kinachotakiwa ni kuhubiri ili watu waokoke.
Alisema kwa ujumla jambo hili ni nyeti kwa kuwa limechanganya wananchi na kwa kuwa kila mtu ana kazi yake, hivyo kinachotakiwa kufanya ni kumwachia Rais na wasaidizi wake, “kutueleza ukweli wa mzee huyu”.
Ahmed Makongo anaripoti kutoka Bunda, kwamba Serikali ya wilaya imelazimika kuruhusu watu 600, badala ya 300 kama ilivyokuwa kawaida, kwenda Loliondo mkoani Arusha, kupata tiba kutoka kwa Mchungaji Mwasapila, kutokana na kuwapo dalili za vurugu katika kituo cha hapa.
Mkuu wa Wilaya, Francis Isaac, alifikia hatua hiyo jana asubuhi, baada ya kuzongwa na mamia ya wananchi kutoka mikoa mbalimbali ya Kanda ya Ziwa, na mingine jirani, wakidai kuwa wamekaa kituoni hapo kwa zaidi ya siku tano, bila kuruhusiwa kwenda kwa Mwasapila.
Wananchi hao wakiwamo zaidi ya wagonjwa 10 waliokuwa na hali mbaya kiafya, kiasi cha kushindwa kusimama na kulazimika kulala kwenye banda linalotoa huduma
ya kusajili magari, walisikika wakisema wamekaa sana hapo na hali zao zinaendelea kuwa mbaya na hivyo wanataka waruhusiwe waende kupata tiba, vinginevyo watafanya vurugu.
0 Comments