Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeibua kashfa zingine alizodai zilisababishwa na watu aliowaita ni mafisadi huku kikitoa siku 90 kwa serikali kueleza zilipo fedha zilizorudishwa na watuhumiwa waliochota mabilioni ya fedha kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Akizungumza katika mkutano wa hadhara kwenye viwanja vya Chipukizi mkoani Tabora, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa, alisema kama serikali haitaeleza zilipo fedha hizo, Chadema kitafanya maandamano nchi nzima kuueleza umma.
Alisema fedha nyingine ambazo serikali inatakiwa kueleza zilipo ni pamoja na zile za Taasisi ya upatu ya Development Entrepreneurship for Community Initiative (Deci), ambazo ni Sh. 14.5 bilioni.
Dk. Slaa alisema fedha nyingine ambazo hazionekani ni Sh. 249 bilioni zilizothibitishwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Alifafanua kwamba awali serikali ilieleza kuanzisha benki ya rasilimali pamoja na benki ya wakulima kwa kutumia fedha za EPA, lakini haijafanya hivyo na fedha hizo hazionekani.
Kuhusu orodha ya mafisadi, aliwataja baadhi ya viongozi wa juu waliokuwa katika serikali ya awamu ya tatu, kwamba ni vinara na kwamba walihusika na uuzaji wa zilizokuwa nyumba za serikali.
Alisema viongozi hao waliuza kiholela nyumba hizo huku wakijua kwamba wanaudanganya umma na kuwaacha watumishi wakiishi hovyo mitaani.
Katika orodha hiyo, Dk. Slaa alimtaja mtumishi mmoja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ambaye alisema ameisababishia serikali hasara ya sh. 800 bilioni kwa kuzuia mali za mfanyabiashara mmoja ambaye baadaye alishinda kesi na kudai fidia ya kiasi hicho cha fedha.
Viongozi wengine walitajwa kwenye orodha hiyo ni pamoja na makada waandamizi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), aliosema wamenufaika na wizi wa EPA pamoja na ofisa mmoja wa Idara ya Usalama wa Taifa.
Aliongeza kwamba hawezi kuogopa kusema ukweli kwa kuhofia kufa na kuacha mali za umma zinaliwa na watu wachache ambao hawana uchungu na Watanzania wenzao ambao wamewakabidhi jukumu la kusimamia mali zao.
Dk. Slaa alisema viongozi hao walijigawia nyumba hizo kwa kisingizio kwamba watajenga nyingine na badala yake wamejenga nyumba 150 jijini Dar es Salaam, ambapo kati ya hizo wamezipangisha na nyingine wameziuza tena.
Kutokana na ufisadi huo serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kwa ajili ya kulipia kodi za nyumba wanazotumia viongozi mbalimbali wakiwemo majaji ambao hulazimika kulala katika nyumba za kulala wageni.
Dk. Slaa aliongeza kuwa viongozi hao kwa pamoja walikiuka Katiba ya nchi waliyokuwa wanaisimamia ambapo katika ibara ya nane inakataza kiongozi wa serikali kutapanya mali za umma.
Mbali ya orodha hiyo, Dk. Slaa alizungumzia ufisadi wa rada na reli ambapo alidai kuwa aliwaeleza serikali matukio hayo lakini wao kwa ujanja ujanja waliwabeza na kukaa kimya hadi kupelekea kuwepo kwa hali ilivyo sasa.
Katika mkutano huo, baadhi ya viongozi wa Chadema walizungumza akiwemo mshauri wa masuala ya sheria wa chama hicho, Mabere Marando, Profesa Abdallah Safari, Fedrick Mpendazoe, Wilfred Lwakatare, Msafiri Mtelemwa na John Mrema.
Viongozi hao watatembelea wilaya zote za mkoa wa Tabora.
Naye Mabere Marando akihutubia katika mkutano huo alisema kuwa anashangaa pale CCM wanapodai kwamba wanajivua gamba wakati chama hicho ndiyo gamba linalotakiwa na Watanzania liondoke badala ya kufukuzana wenyewe kwa wenyewe.
Marando amesema yeye kama wakili yupo tayari kusimami kesi ya mafisadi wa fedha za kampuni ya Kagoda na kwamba anafahamu wahusika wakuu japo serikali inadai haiwafahamu.
0 Comments