Wakazi wa Mjimwema Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam wamekuja juu na kuipa Serikali siku saba iwe imefunga Hoteli ya Kitalii ya South Beach na kumuondoa mwekezaji anayetuhumiwa kufanya mauaji ya mwenzao, Lila Hussein (34), vinginevyo wataitisha maandamano makubwa ya vijana ili kuichoma moto.
Hatua hiyo ya wananchi imefikiwa siku chache baada ya kijana huyo ambaye ni mkazi wa eneo hilo kudaiwa kuchomwa moto na mmiliki wa hoteli hiyo, Salim Chipata (53), na kumsababishia majereha mwilini mwake kabla ya kifikwa na mauti mwishoni mwa wiki iliyopita akiwa amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Wakizungumza katika kikao cha pamoja na uongozi wa mtaa wa Mjimwema kilichofanyika jana Kigamboni, wananchi hao walisema wamechoshwa na vitendo vya kikatili vinavyofanywa na mwekezaji huyo ambavyo vinakiuka haki za binadamu.
“Kila mara tunaokota maiti jirani na hoteli hii ya South Beach na sisi tunadhani huyu mmiliki wake anajua vifo hivi vinatokana na nini, hivyo hili tukio la sasa la mauaji ya kuchomwa moto hatutakubali lipite hivi hivi,” alisema mmoja wa wakazi hao.
Akizungumza katika kikao hicho kilichohudhuriwa na wananchi wa eneo hilo pamoja na maofisa wa Kituo Cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) cha jijini Dra es Salaam, Ali Seleiman Mwambogo (83), alisema suluhisho la matatizo yanayoendelea kutokea katika hoteli hiyo ni kuifunga.
Alisema kama Serikali haitasikiliza kilio chao na kuifunga hoteli hiyo, wao watahamasisha vijana ili waivamie na kuichoma moto kwa madai kuwa mmiliki wake ameua kijana wao ambaye hakuwa na hatia yoyote.
Alilalamika kuwa Serikali ina kawaida ya kuwasikiliza wawekezaji kuliko wananchi wake na kwamba kama itatokea ikafanya hivyo ijiandae kushuhudia maafa makubwa katika eneo hilo.
Alishauri kuwa licha ya hoteli hiyo kufungwa, pia itaifishwe na kupewa mtu mwingine ambaye atakuwa na moyo wa kibinadamu anayeweza kushirikiana na wananchi wanaoizunguka eneo hilo.
Mkazi mwingine wa eneo hilo, Mohamed Athumani (75), akizungumza katika kikao hicho alisema lazima walipize kisasi kwa kuwa ndugu yao ameuawa kikatili kwa kuchomwa moto na mwekezaji huyo bila hatia.
Aliitaka Serikali itafute mahali pa kumpeleka mwekezaji huyo vinginevyo wananchi wataungana na kwenda kuiteketeza kwa moto.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mjimwema, Mwinyi Baishi, aliungana na wananchi wake na kuiomba Serikali kuwasaidia kwa kuifunga hoteli hiyo ili kuepusha maafa makubwa ambayo yamepangwa kufanywa na wananchi baada ya siku saba kupita.
Alisema baada ya mwekezaji huyo kudaiwa kusababisha mauaji hayo, Serikali ifuatilie ili kuona kama bado ana uhalali wa kuendelea kuwa mwekezaji anayemiliki hoteli ya kitalii.
Hivi sasa hoteli hiyo inalindwa na askari polisi wenye silaha baada ya mmiliki wake kushikiliwa na vyombo vya dola kwa tuhuma za kusababisha mauaji ya Lila.
Anadaiwa kummwagia petroli Lila na kumchoma moto baada ya kumtuhumu kuzamia kwenye muziki wakati wa usiku katika hoteli hiyo bila kutoa malipo.
Chipata alipandishwa kizimbani juzi katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke akikabiliwa na mashtaka ya mauaji ya kumchoma moto Lila.
Mtuhumiwa huyo mkazi wa Mikocheni A, alifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Temeke, Khasim Mkwawa, akiwa pamoja na mshtakiwa mwenzake, John Mwangiombo (32), kujibu mashtaka hayo.
Mwendesha Mashtaka, Inspekta wa Polisi, Dustan Kombe, aliiambia mahakama hiyo kuwa Aprili 10, mwaka huu, saa 6:30 usiku eneo la Mjimwema Kigamboni, washtakiwa walishirikiana kumpiga na kumchoma Lila na kumsababishia kifo.
CHANZO: NIPASHE
Hotel ya South Beach kwa ndani jinsi inavyoonekana.
0 Comments