WAZAZI wametakiwa kutokuwapa watoto wao vidonge vya uzazi wa mpango ili kuzuia tatizo la
upatikanaji wa mimba kwani kwa kufanya hivyo hawatamsaidia mtoto zaidi ya kumjengea
mazingira ya kutokusoma na kupata maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU).

Wito huo umetolewa hivi karibuni na Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete wakati alipokuwa anazungumza na wakazi wa wilaya ya Nanyumbu mara baada ya kujulishwa na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali mstaafu Anatory Tarimo kwamba hivi sasa tatizo la mimba katika mkoa huo limepungua na kuna tetesi kuwa kuna baadhi ya wazazi wanashirikiana na watoto wao kuwapa vidonge vya kuzuia mimba
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) aliwasisitiza wazazi hao kufahamu kuwa jukumu walilonalo ni kuhakikisha kuwa watoto wao wanasoma na kuepuka mazingira ambayo yatawasababishia kupata mimba na hivyo kukatiza masomo yao.

Kwa upande wa wanafunzi Mwenyekiti huyo wa WAMA aliwataka kusoma kwa bidii na si kutumia uzazi wa mpango kwani uzazi wa mpango ni kwa watu ambao wameolewa na si wao, nao wakati wao ukifika watautumia hadi wachoke. Pia aliwataka wakumbuke kuwa hakuna dini ambayo inaruhusu watu kufanya tendo la ndoa kabla ya kufunga ndoa.

Naye Mkuu wa Mkoa huo Kanali Mstaafu Anatory Tarimo, alisema kuwa hivi sasa tatizo la
mimba limepungua kwani kwa mwaka 2007 wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari waliopata ujauzito walikuwa ni 530 kati ya hao, 104 walitoka katika wilaya ya Nanyumbu.

“Mwaka 2007 watoto waliopata ujauzito, wanafunzi wa shule za msingi walikuwa 48 na sekondari 56 na kwa mwaka 2010 tatizo lilipungua, kwani wanafunzi wa shule ya msingi
walikuwa tisa na sekondari walikuwa wawili,” alisema Kanali mstaafu Tarimo.

Aliendelea kusema kuwa, kuna tetesi kwamba tatizo hili limepungua kutokana na baadhi wa wazazi kuwapa watoto wao vidonge vya kuzuia mimba pia kuna baadhi ya wao wenyewe
wanafunzi wanatumia vidonge hivi ili wasipate ujauzito.(Full story na Habari leo)