RAIS Jakaya Kikwete ameungana na Watanzania wengine kuwalilia marehemu wa ajali ya
basi la Ngorika na `daladala’ aina ya Hiace iliyotokea Ijumaa asubuhi eneo la Makumira, wilayani
Arumeru, Arusha na kusababisha vifo vya watu kumi papo hapo.

Kutokana na msiba huo, Rais Kikwete Jumamosi alitumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Isidori Shirima, akisema; “Nimesikitishwa na kuhuzunishwa sana kutokana na ajali hiyo mbaya ya barabarani ambayo kwa mara nyingine imepoteza maisha ya watu wetu 10 wasio na hatia.

“Kupitia kwako wewe Mkuu wa Mkoa, ninatuma salamu za rambirambi kwa familia, ndugu
na jamaa waliopotelewa na wapendwa wao katika ajali hii mbaya, hivyo namwomba
Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aziweke mahali pema peponi roho za marehemu wote,
Amina.
 
Rais Kikwete pia amesema anamuomba Mwenyezi Mungu awajalie wafiwa wote moyo wa
uvumilivu, ujasiri na subira wakati huu wanapoomboleza vifo vya wapendwa wao na kusema kwamba yeye binafsi yupo pamoja nao katika muda wote wa maombolezo.

Kwa upande mwingine, Rais Kikwete amewaombea kwa Mwenyezi Mungu watu wote waliojeruhiwa katika ajali hiyo ili wapone haraka na kurejea katika hali zao za kawaida ili hatimaye waweze tena kuungana na familia, ndugu, jamaa na marafiki zao.