MADAKTARI wanafunzi wamesema mfumo mbovu wa mazingira ya kazi kwa madaktari nchini, unawakatisha tamaa na kuwachochea kuendelea kukimbilia nje ya nchi kutafuta maslahi mazuri, baada ya kumaliza masomo yao.

Hali hiyo pia wamesema inachochewa na mazingira duni ya kazi na maisha mabovu waliyonayo madaktari walio kazini, ambayo kwao ni dira ya wanakoelekea ambayo imekuwa ikiwakatisha tamaa vile vile.

Aidha, wameitaka Serikali kuimarisha miundombinu ya afya, maslahi kwa madaktari na kuimarisha sekta ya utafiti wa tiba nchini, ili kuboresha huduma za afya kwa kuvumbua dawa mpya na kuongeza ufanisi kwa madaktari katika taaluma yao, ikiwa ni hatua ya kupambana na wimbi la kukimbia nchi.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam katika semina
ya siku mbili ya Utafiti kwa Madaktari Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba (MUHAS), Viongozi wa Chama cha Madaktari Wanafunzi Tanzania (TAMSA), Tawi la MUHAS, walisema mfumo wa afya unawakatisha tamaa.

“Hakuna matumaini kwa madaktari walioko kazini, maisha yao yanatukatisha tamaa kabisa, wengine wanafanya hata biashara za magendo kukidhi mahitaji, sisi tunasoma miaka
mitano hapa, lakini maisha yetu baada ya masomo kwa kipato ukiyalinganisha na aliyesoma shahada kwa miaka mitatu chuo kikuu kingine, ni tofauti kabisa,” alilalamika Asilia Peter.

Peter ambaye ni Mwenyekiti wa TAMSA - MUHAS na Makamu wa Rais wa Bodi ya TAMSA Taifa, alisema madaktari walioko kazini, wanafanya kazi kama wamekata tamaa na mfumo uliopo hauwavutii kuendelea kufanya kazi nchini, hivyo wataendelea kukimbilia nje.

“Sekta ya afya ni ya muhimu kwa Taifa lolote, watu kama hawana afya hakuna uzalishaji, lakini vituo vya kazi wanavyopangiwa madaktari huko mikoani ni balaa tupu, hakuna vifaa vya kazi, dawa, nyumba za kuishi wala shule, unakuta daktari ana familia, anakwenda kuishi namna gani? Hali si nzuri na wataendelea kuikimbia nchi tu,” alisema Peter.

Alishauri Serikali kutia mkazo mkubwa katika sekta ya afya kwa kuboresha maslahi ya madaktari, miundombinu na motisha kwa wanaopangiwa kazi vijijini, zaidi ya ilivyo sasa, ili kukabiliana na wimbi la madaktari kukimbia.

Tatizo la madaktari kukimbia nchi limekuwa kubwa ambapo wengi wao hukimbilia Botswana na Afrika Kusini kufanya kazi ambako inadaiwa maslahi ni bora kuliko nchini.

Lakini Mwenyekiti wa Kamati ya Utafiti na Tiba ya Chama cha Wanafunzi Madaktari Tanzania (SCOMER), Thuraiya Hashim, alisema pamoja na changamoto ya kimfumo inayolikabili Taifa, ni vyema madaktari watangulize uzalendo na kukubali ukweli kuwa maslahi si mazuri kutokana na umasikini.

“Ni kweli madaktari wanafunzi na kamili hawaoni nafasi ya kipaumbele kufanya kazi nchini, wanatafuta maslahi nje na wanayapata ila kubwa zaidi ni uzalendo, kwani nyumbani ni nyumbani tu, lakini naiomba Serikali isifanye kama haioni tatizo, iboreshe mazingira ya kazi na kuwahakikishia ajira za moja kwa moja wanafunzi madaktari wanaomaliza masomo,” alishauri Hashim.

Akizungumzia semina hiyo iliyofanyika jana na nyingine Jumamosi ijayo, Hashim alisema lengo kuu ni kuwasaidia wanafunzi madaktari kuelewa zaidi umuhimu wa utafiti katika taaluma yao, hasa kuhusu dawa mbalimbali na kujua kuwa utafiti ni maisha ya daktari na si somo la kufanyia mtihani na kufaulu tu.

Alisema wanafunzi waliojitokeza ni zaidi ya 120 wakati uwezo wao ulikuwa 60 hali inayodhihirisha kuwa, wanafunzi madaktari wanahitaji kujua zaidi kuhusu utafiti, hivyo Serikali inapaswa kuboresha sekta ya utafiti katika tiba kuanzia shuleni, vyuoni na kazini.

Aliiomba pia Serikali kutafuta kila mbinu kukabiliana na uhaba wa madaktari nchini. Awali akifungua semina hiyo, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo cha MUHAS, Taaluma, Utafiti na
Ushauri, Profesa Eligius Lyamuya, ambaye pia ni mlezi wa TAMSA, alisema utafiti ni kiini cha ugunduzi wa tiba bora na husaidia katika elimu zaidi ya nadharia darasani.

Katika hatua nyingine, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imewataka madaktari wote bingwa
waliopangiwa vituo vya kazi kwenda mara moja walikopangiwa kufanya kazi , la sivyo hatua kali za kinidhamu ikiwamo kufutiwa usajili zitachukuliwa dhidi yao.

Kwa mujibu wa tangazo maalumu lililotolewa na wizara hiyo na kusainiwa na Katibu Mkuu, Blandina Nyoni, wahusika ambao hawajaenda kwenye vituo walivyopangiwa, wanatakiwa kwenda kuanza kazi katika vituo hivyo mara moja, kama barua zao zinavyoelekeza.

Taarifa hiyo ilisema Serikali kupitia wizara hiyo, imewadhamini na kuwalipia gharama za
mafunzo madaktari wa uzamili na uzamivu walioajiriwa na Serikali na hospitali binafsi na wanaochukua mafunzo hayo katika vyuo binafsi nao pia wanalipiwa na Serikali, ili kuongeza idadi ya madaktari bingwa nchini na kusogeza huduma zao karibu na wananchi.

“Baada ya kumaliza mafunzo yao, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, iliwapangia vituo vya kazi. Madaktari wengi, wamekwishaanza kazi katika vituo walivyopangiwa. Hata hivyo, wapo ambao hawajaenda katika vituo walivyopangiwa, bila sababu zinazokubalika.

“Kwa tangazo hili, yeyote atakayekiuka agizo la barua na tangazo hili kutofanya kazi, atachukuliwa hatua za kinidhamu, ikiwa ni pamoja na kusimamishwa usajili wake na hata kufutwa katika Daftari la Usajili na kuwataka madaktari ambao hawajapokea barua wawasiliane na Wizara mara moja.