Baraza la Maadili jana liliendelea kuwahoji vigogo ambao hawajawasilisha matamko ya mali zao wakiwemo Mhasibu Mkuu wa Ikulu Joseph Sanga na Mwandishi wa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Said Nguba.
Akisoma mashitaka yanayowakabili, Mwanasheria wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Getrude Cyriacus, alisema viongozi hao wamekiuka sheria ya maadili inayowataka kuwasilisha kwa sekretarieti ya maadili matamko ya mali zao.
Jana walioanza kuhojiwa mi Nguba ambaye alidai kuwa kwa septemba 2008 alikuwa mgonjwa kwa miezi 3 na kuwa nje ya ofisi.
Alisema hata alipowasili ofisini kwake hakujua kama alihitajika kujaza fomu na ofisi yake kushindwa kumpa taarifa za aina yoyote kuhusu fomu hizo.
Nguba alisema hata mwaka 2009 hakuweza kujaza fomu hizo kutokana na kuwa na vikao nje ya ofisi kwa kipindi kirefu.
“Ni kweli nilipata fomu, lakini katika mwaka huo nilikuwa mkoani Dodoma kuhudhuria vikao na hata nilipowasili ofisini kwangu sikuambiwa chochote kama kuna fomu ya maadili ninayohitajika kuijaza,” alisema.

Mwenyekiti wa Baraza hilo, Jaji Damian Lubuva alisema sababu ya kusafiri haina uzito kwa kuwa kuna viongozi wengi wanasafiri na wanajaza fomu na kumtaka aonyeshe uthibitisho ambapo Nguba hakuwa navyo kwa wakati ule na kuomba Baraza hilo limpe muda ili aweze kuwasilisha taarifa hizo.
Mwingine ni Mhasibu Mkuu wa Ikulu Joseph Sanga, ambaye anadaiwa matamko ya miaka 3 kuanzia 2007 hadi 2009 ambapo Tume ilimtumia barua na fomu kwa ajili ya kujaza.
Sanga alisema kuwa alipopata hati ya kuitwa alishitukaambapo aliamua kufuatilia masjala na kubaini kuwa fomu zake hazikumfikia na kuamua kufuatilia tume na kuambiwa anastahili kujaza na akapewa fomu hizo.

Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Ndani katika Mamlaka ya Chakula na Lishe, Guido Leshabari, alipotakiwa kutoa maelezo kwanini hakuwasilisha matamko ya mali zake tangu mwaka 2007 licha ya kupelekewa barua, alidai alichanganyikiwa na kuuguliwa na kaka yake.
Alisema alipata fomu ikimtaka azijaze, lakini alishindwa kwani alichanganyikiwa kutokana na kuuguliwa kwa muda mrefu.
Majibu hayo hayakuwaridhisha majaji hao ambao walimhoji alishindwaje kujaza fomu hizo ingawa alikuwa anakwenda kazini kama kawaida pamoja na kuuguliwa.
Jaji: Unasema ulikuwa unauguliwa, inamaana kazini ulikuwa unakwenda kama kawaida wakati huo.
Leshabari: Ndio nilikuwa nakwenda kama kawaida.
Jaji: Inamaana huko kazini kazi zako ulikuwa unaharibu haribu kwasababu umechanganyikiwa kutokana na kuuguza?
Leshabari: Hapana nilikuwa nafanya kazi zangu kama kawaida.
Jaji: inamaana kwenye kujaza fomu za maadili tu ndio ulikuwa unachanganyikiwa?
Leshabari: Hapana.
Mwingine aliyehojiwa ni Meneja Ukaguzi wa Hesabu za Ndani katika Mamlaka ya Maji Safi (Dawasco),Rosemary Lyamuya, ambaye muda mwingi ulitumika kulumbana na mawakili wa sekretarieti hiyo kuhusu cheo chake.
Sekretarieti hiyo ilimwita kama Mkuu wa Ukaguzi wa Hesabu za Ndani Dawasco wakati yeye akidai kuwa hicho sio cheo chake.
Lyamuya alikuwa akiwaeleza kuwa aliajiriwa kwa cheo cha meneja ukaguzi wa hesabu za ndani na si Mkuu wa hesabu za ndani jambo ambalo lilidumu kwa muda mrefu.
Lyamuya alisema alipopelekewa fomu za kujaza mali zake hakujua kama kwa nafasi aliyonayo anawajibika kufanya hivyo na aliomba baraza hilo limsamehe kwa kutokujua alichotakiwa kufanya.