Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetaja viongozi wake wakuu watakaoongoza maandamano ya amani yaliyopangwa kufanyika katika mikoa 10 ya Tanzania Bara, Jumamosi wiki hii.
Maandamano hayo yanalenga kuishinikiza serikali, pamoja na mambo mengine, kubadilisha Muswada wa Sheria ya Marejeo ya Katiba wa Mwaka 2011.
Pia, kuitaka serikali kutoa muda kwa wananchi kushauriana, kujadiliana na kutoa maoni kabla muswada haujafikishwa bungeni; na muswada kuandikwa kwa lugha ya Kiswahili.
Mkuu wa Operesheni hiyo, Singo Kigaila, aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuwa maandamano hayo yataongozwa na timu 10 tofauti zitakazojumuisha viongozi wakuu wa kitaifa, wabunge, wajumbe wote wa Kamati Kuu (CC) na wa sekretarieti ya chama katika mikoa ya Arusha, Mbeya, Kigoma, Kilimanjaro, Ruvuma, Dodoma, Pwani, Mtwara, Tabora na Morogoro.
Alisema timu ya Mbeya, itaongozwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, akishirikiana na Mjumbe wa CC na Mbunge wa Viti Maalum, Chiku Abwao; Mjumbe wa CC na Mbunge Viti Maalum, Naomi Kaihula; Mbunge wa Mbozi Magharibi, David Silinde; Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama, Wilfred Lwakatare, na Thomas Nyimbo.
Timu ya Tabora, itaongozwa na Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa, akishirikiana na Mjumbe wa CC na Mwenyekiti wa Baraza la Wazee, Nyangaki Kilungushela; Mjumbe wa CC na Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa; Mbunge Viti Maalum, Lucy Owenya; Mbunge Viti Maalum, Anna Maulida Komu; Mkurugenzi wa Bunge na Halmashauri, John Mrema na Fred Mpendazoe.
Timu ya Morogoro itaongozwa na Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara ambaye pia ni Mbunge wa Mpanda Mjini, Said Arfi; akishirikiana na Mjumbe wa CC, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema Mkoa huo na Mbunge wa Viti Maalum, Suzan Kiwanga; Afisa Ulinzi na Usalama, Hemed Sabula; Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Hamad Musa Yusufu; Mbunge Viti Maalum, Mariam Msabaha; Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda; na Mbunge Viti Maalum, Christowaja Mtinda.
Timu ya Pwani itaongozwa na Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Saidi Issa Mzee; akishirikiana na Mbunge wa Mbulu, Mustapha Akunaay; Mbunge Viti Maalum, Anna MaryStella Mallac; Mbunge wa Biharamulo Magharibi, Dk. Antony Mbassa; Mbunge Viti Maalum, Conchesta Rwamlaza; Mbunge Viti Maalum, Christina Lissu; na Afisa Mwandamizi Sheria na Haki za Binadamu, .
Timu ya Arusha itaongozwa na Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe; akishirikiana na Mjumbe wa CC na Mbunge Viti Maalum, Grace Kihwelu; Mwenyekiti Mkoa huo, Samson Mwigamba; Mbunge wa Ilemela, Higness Kiwia; Mbunge wa Maswa Mashariki, Sylvester Kasulumbayi; Mbunge Viti Maalum, Raya Ibrahim; na Profesa Abdallah Saffar.
Timu ya Mtwara itaongozwa na Mjumbe wa CC, Mabere Marando; wakati ya Kilimanjaro itaongozwa na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu; ya Kigoma itaongozwa na Mbunge wa Nyamagana, Ezekia Wenje; ya Dodoma itaongozwa na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema; na ya Ruvuma itaongozwa na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika.
Kigaila, ambaye ni Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo wa Chadema, alisema tayari wamekwisha kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi na kuwataka wananchi wa mikoa hiyo kujiandaa kwa ajili ya maandamano hayo.
Alisema hawatakwenda katika mikoa ya Kanda ya Ziwa inayojumuisha mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Mara na Kagera kwa vile wamekwisha kwenda huko, hivyo wananchi wa mikoa hiyo watajiunga nao katika maandamano ya sasa.
Kigaila alisema wanataka muswada huo ubadilishwe kwa kuzingatia maoni ya wadau ili kazi ya kuandika Katiba mpya iondolewe mikononi mwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ikabidhiwe kwa umma.
“Maana yake Katiba ni mali ya umma, kama Ibara ya 8 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya sasa inavyotamka,” alisema Kigaila.
Alisema Watanzania hawawezi kwenda kuandika Katiba kwa hati ya dharura kwani hawako vitani na hawatoki vitani, na kwamba, hatua hiyo inanyima wananchi uhuru wa kutoa maoni.
“Tunataka muswada huu uondolewe, suala lirudishwe kwa wananchi, watoe maoni yao, washauriane, wapendekeze muswada wanaoutaka, upelekwe bungeni watu wakiwa wametoa maoni,” alisema.
Alisema wanataka muswada huo uandikwe kwa Kiswahili kwa sababu Watanzania zaidi ya asilimia 80, wameishia elimu ya msingi, ambayo lugha ya kufundishia ni Kiswahili, pia wanaongea Kiswahili na lugha zao za makabila, hivyo hawawezi kuchangia muswada huo kwa vile umeandikwa kwa lugha ya Kiingereza.
Kigaila alisema licha ya Rais Jakaya Kikwete kutamka kuridhia mabadiliko ya Katiba, vitendo vilivyojitokeza baadaye, imebainika kuwa serikali haina nia ya kuandikwa Katiba Mpya.
Alisema ushahidi wa hilo, ni matamshi yaliyowahi kutolewa na Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema kwamba, haiwezekani kuandikwa Katiba Mpya.
Kigaila alisema ushahidi mwingine, ni jina la muswada wenyewe, kuitwa “Muswada wa Marejeo ya Katiba”, ambalo alisema linamananisha “kupitia kwa lengo la kufanya masahihisho” na si kuandika Katiba Mpya kama wanavyotaka Watanzania.
Alisema jambo lingine ni kitendo cha muswada kuuweka umma pembeni na kukabidhi mchakato wa kuandika Katiba chini ya wanachama watatu wa CCM; Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Serikali ya Mapinduzi (SMZ) na Waziri wa Katiba na Sheria, ambao alisema ndio watakaowaamulia Watanzania kupata Katiba ya aina gani.
Kigaila alisema Rais wa Jamhuri ya Muungano, ambaye ni Mwenyekiti wa CCM atakuwa na kazi ya kuteua tume ya kushughulikia mchakato wa mabadiliko ya Katiba, kuandaa hadidu za rejea, kupokea ripoti ya tume na kuamua ripoti hiyo ipelekwe kwenye Baraza la kuandika Katiba.
Alisema Rais wa SMZ, ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar atashauriana na Rais wa Jamhuri ya Muungano, kupokea nakala ya ripoti ya tume; na kwamba, mwanachama watatu wa CCM, ambaye ni Waziri wa Katiba na Sheria, ndiye atateua wajumbe wa sekretarieti ya tume na kuamua mishahara ya tume.
0 Comments