Mbunge wa Arusha Mjini kwa tiketi ya Chadema, Godbless Lema, jana alisababisha kizaa zaa katika manispaa ya Iringa baada ya mamia ya wananchi kumsindikiza kwa maandamano alipomaliza mkutano wake.
Mbunge huyo ambaye aliambatana na mbunge wa Mbeya Mjini kwa tiketi ya chama hicho, Joseph Mbilinyi, waliwapa wakati mgumu makachero wa Polisi na Usalama wa Taifa kuzuia maelfu ya wakazi hao waliokuwa na shauku ya kuambatana na wabunge hao wawili.
Hali hiyo ilijitokeza mara baada ya kuwasili kwa wabunge hao na kuzungumza na maelfu ya wakazi wa mji huo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya soko la Kihesa ambapo Lema aliwataka wananchi kutofanya maandamano lakini anayetaka kuongozana naye anaweza kufanya hivyo.
Wakati Lema akiwahutubia wananchi hao, alisema baada ya kumaliza mkutano huo angetembea kwa miguu katika viunga vya Manispaa hiyo kwa lengo la kujifunza mambo mbalimbali na kuwataka wananchi wanaoelekea maeneo ya katikati ya mji kufuatana naye lakini wasifanye maandamano.
Baada ya kutamka kauli hiyo, makachero wa Polisi walionekana kutotulia eneo moja na kutuma ujumbe kwa baadhi ya viongozi wa Chadema wakimsihi Lema na wenzake kutotembea kwa miguu na badala yake wapande magari.
Hata hivyo, Lema alisisitiza kwamba anachotaka kufanya si maandamano bali ni kutembea kwa miguu na kwamba kama kulikuwa na wananchi wanaelekea anakokwenda wafuatane naye na kuwataka Polisi kuwa wapole.
“Jamani sitaki wananchi muandamane ila mimi nimesema nitatembea kwa miguu kuelekea huko mjini, kama kuna anaelekea huko basi twende pamoja lakini msifanye vurugu na mkae nyuma yangu, niacheni mimi nikaembele,” alisema Lema na kushangiliwa na wananchi.
Kauli hiyo iliwafanya makachero hao kuwasiliana na wenzao kuomba ulinzi zaidi ambapo magari matano yaliyosheheni askari wa kikosi cha kutuliza ghasia yaliwalisi eneo la mkutano.
Hali hiyo ilionekana kumchanganya mbunge huyo na kuamua kutembea kipande kifupi tu kutoka eneo la mkutano hadi eneo la Majembe kabla ya kupanda gari ambalo hata hivyo wananchi walianza kulisukuma na askari wa kikosi cha kutuliza ghasia kutanda barabara nzima wakiwa kwenye magari maluum kuimarisha usalama huku wakijihami kwa kupiga picha.
0 Comments