Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Dk. Kofi Annan, amesema Tanzania inayo fursa ya kunufaika na soko kubwa la chakula duniani, ikiwa itawekeza zaidi kwenye uzalishaji wa mazao ya chakula, hasa kwa kuwatumia wakulima wadogo vijijini.
Dk. Annan, aliyasema hayo jana, wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Iyula, wilayani Mbozi, alikokwenda kutembelea duka la dawa za kilimo na mifugo lililoanzishwa kijijini hapo kwa ufadhili wa Shirika la Alliance for Green Revoluion in Africa (AGRA), ambalo yeye ni Mwenyekiti wake.
Alisema kwa kuwa wakati huu dunia nzima inatafakari juu ya uhakika wa upatikanaji wa chakula, Tanzania inaonekana kuwa na fursa muhimu ya kuzalisha chakula cha kujitolesheza yenyewe na ziada ikauza nchi nyingine na kujipatia faida kubwa.
Alisema shirika lake linafanya kazi na wakulima wadogo nchini ili kuwapatia ujuzi wa kuzalisha mazao mengi, lengo likiwa ni kuwaongezea tija na kipato wakulima hao.
Dk. Annan alieleza kuwa, yeye na ujumbe wake wameridhishwa kwa kiasi kikubwa na hali ya uzalishaji wa mazao katika wilaya za Mbeya Vijijini na Mbozi, hivyo shirika lake linahitaji kufanya kazi kwa karibu na serikali ya Tanzania ili kuongeza mara dufu uzalishaji wa mazao.
"Lengo kubwa ni kuwawezesha wakulima kuendesha kilimo chenye tija, hili litawezekana kwa wao kuwatumia vema wataalamu wa kilimo kuendesha kilimo cha kisasa," alisema Dk.Annan.
Aliongeza kuwa ujumbe wa AGRA, una wajumbe wa Bodi kutoka Marekani, Uholanzi, Ethiopia na Kenya na kwamba umekuja nchini katika mkoa wa Mbeya kwa ajili ya kujionea hatua iliyofikiwa katika uendelezaji wa kilimo.
Akiwa Jijini Mbeya, Dk. Annan, pia alipata fursa ya kutembelea skimu ya umwagiliaji ya Iganjo na kupewa nafasi ya kuzungumza na kuwauliza maswali baadhi ya wakulima wa bonde la Uyole.
0 Comments