Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Chadema), ameihoji serikali kwanini isipeleke vifaa vya studio ya muziki kwa Baraza la Taifa la Sanaa (BASATA) ili wasanii wengi waweze kuitumia.
Mbilinyi maarufu kama Sugu, alihoji suala hilo bungeni juzi wakati akiuliza swali la nyongeza, ambapo alisema kuwa Flava Unit iliyokabidhiwa studio hilo ni kampuni binafsi.
Akijibu swali hilo, Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Dk. Emmanuel Nchimbi alisema hilo ni jambo jema bali watatafuta chombo kingine cha kusimia badala ya BASATA.
Katika swali la msingi Mbunge wa Viti Maalum, Martha Mlata, alisema Rais alitoa kwa Clouds FM Mastering Machine ili kuwasaidia wasanii kupunguza tatizo la kazi zao.
Alitaka kujua ni wasanii wangapi wamenufaika na wanafaidikaje.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenela Mkangala, alisema mastering studio hiyo haikutolewa kwa Clouds bali imetolewa kwa kikundi cha wasanii waliojiunga pamoja na kuanzisha chama cha Tanzania Flava Unit.
Alisema wasanii hao ni wale wa Tanzania House of Talent (THT) na baadhi ya wanamuziki wa kizazi kipya ambao wanaushirikiano wa karibu sana wa kiutendaji na kituo cha radio cha Clouds FM kinachomilikiwa na Ruge Mutahaba.
Dk. Mkangala alisema studio hiyo bado haijaanza kufanya kazi na hivyo ni mapema kuelezea jinsi wasanii walivyonufaika.
Alisema ufungaji wa studio hiyo utakapokamilika wasanii watanufaika kwa kutumia kuzalisha kazi zao kwa gharama nafuu.(source Nipashe)
0 Comments