Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) jana waliuchoma moto muswada wa sheria ya kuanzisha Tume ya mapitio ya Katiba Tanzania katika mkutano wa hadhara mjini hapa.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Hamad Mussa Yussuf, aliongoza uchomaji moto huo saa 11:40 jioni pale alipoagiza kupelekewa taa na kiberiti kwa nia ya kuanza kuuchoma ambapo wafuasi wa chama hicho walianza kushangilia.
"Nauchoma muswada huu ambao hauna maana kwa Wazanzibari au mnasemaje... lete kiberiti tuuchome, muswada huu haufai kabisa,” alisema.
Mkutano huo ulifanyika katika viwanja vya Kibandamaiti Mkoa wa Mjini Magharibi, ulikuwa na lengo la kuwaeleza wananchi mchakato wa Katiba mpya Tanzania na rasimu ya muswada wa sheria ya Tume ya mapitio ya Katiba wa mwaka 2011 ambao umepangwa kuwasilishwa bungeni katika mkutano unaoendelea.
Kiongozi huyo alimshambulia kwa maneno makali Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, akidai amekuwa akishiriki kuikandamiza Zanzibar tangu alipolikuwa Waziri wa Katiba na Sheria wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1995 hasa pale aliposimama kidete kuunga mkono mabadiliko ya 11 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya kufutwa Rais wa Zanzibar kutokuwa Makamu wa Rais wa Tanzania.
“Huyu Samuel Sitta amekuja Zanzibar kutuletea muswada huu mchafu ambao umejaa kasoro nyingi na usiokuwa na tija kwa Wazanzibari, ni huyu huyu kama mtakumbuka ndio aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria wakati ule aliyesimama kidete na wenzake kuiondoa nafasi ya Rais wa Zanzibar kutokuwa Makamu wa Rais wa Tanzania, leo anakuja tena na jambo hili,” alisema.
Kuchomwa kwa muswada huo ni mwendelezo wa visa na vituko vinavyoendelea wakati huu wa mchakato wa kuandaa Katiba mpya ifikapo mwaka 2014.
Juzi, Sheikh Farid Hadi aliuchana muswada huo mbele ya Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Haile Sellasie Mjini Zanzibar.(picha haihusiani na tukiona habari kamili toka gazeti la Nipashe)