MWENYEKITI wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa, Augustino Mrema, amewataka Watanzania wajitokeze kuwafichua mafisadi wanaotafuna fedha za miradi ya maendeleo katika halmashauri nchini badala ya kutoa kauli za kumpaka matope Rais Jakaya Kikwete pamoja na CCM.

Mbunge huyo wa Vunjo mkoani Kilimanjaro, alisema hayo mwishoni mwa wiki kwenye mkutano ulioandaliwa na Taasisi ya Alshabab Islamic Daawah ya Morogoro, uliolenga kujadili amani na kuenzi ili kuwawezesha Watanzania kuendelea kuishi na amani.

“Wananchi hatuchukui hatua za kuwataja wezi wa fedha zinazopelekwa na Serikali Kuu kwenye halmashauri zetu.

Tumebaki kuwa watazamaji wakati nchi ikiendelea kuangamia…wananchi wanampaka Rais matope, wanakipaka Chama Cha Mapinduzi matope, lakini wezi tunao na hatuwachukulii hatua za kisheria,” alisema Mrema ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP).

“Halmashauri zinaendeshwa na wezi wa kupindukia, watu wanaichukia Serikali ya Rais Kikwete…watu wanaimba Dowans, lakini hatujachukua hatua za wezi wa fedha za halmashauri zetu.

Rais anaendelea kupata lawama licha ya fedha nyingi kuelekezwa kwenye halmashauri.” “Sasa ni wakati wa kuniunga mkono katika vita hii,” alielezea mwanasiasa huyo.

Kauli ya Mrema ameitoa baada ya Kamati yake kukabidhiwa taarifa ya Mkaguzi na Mdhitibi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2007/2008 na 2009; ambayo ndani yake Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa mkoani hapa, imehusishwa na ubadhirifu mkubwa wa mamilioni ya fedha kupitia Idara ya Fedha.

Akizungumzia halmashauri hiyo ya Kilosa baada ya kupitia taarifa ya ukaguzi wa hesabu uliofanywa na CAG, katika kipindi hicho, kuwa kiasi cha mapato halali ya Sh milioni 727.5 ya makusanyo ya ushuru wa tozo la asilimia tano kwa kila tani ya miwa kutoka Kiwanda cha Sukari Kilombero zimetafunwa.

Kwa mujibu wa Mrema, watumishi wa Idara ya Fedha walikula njama kwa kupunguza tozo la ushuru na kuwa asilimia mbili, hivyo kwa kipindi hicho ilitakiwa kukusanya Sh milioni 785.7, lakini kwa udanganyifu huo, Halmashauri ilikusanya Sh milioni 58.2 na Sh milioni 727.5 kuingia mifukoni mwa watumishi wasio waaminifu.

Alisema ubadhirifu wa aina hiyo unafanyika katika halmashauri nyingi nchini na kuongeza kuwa mbali na wizi huo wa udanganyifu, Idara ya Fedha ya Kilosa, kupitia taarifa ya CAG, ilibainika watumishi wake walikuwa wakijilipa posho ya usafiri hali wakiwa maofisini.

Alisema katika kipindi cha mwaka 2007/2008 na 2009, watumishi hao walijilipa kwa kusaini hati za malipo ya posho zenye kufikia Sh milioni 63.4 ambapo pia watumishi wa Idara hiyo ya Fedha walijilipa kupitia akaunti mbalimbali za watumishi waliostaafu, kuacha kazi na waliofariki kufikia Sh milioni 64.7, baada ya kubainika kuwa mishahara hiyo haikurudishwa Hazina na ilikuwa ikiendelea kulipwa kwenye akaunti hizo.