RAIS Jakaya Kikwete amesema amepata moyo mpya wa kuendeleza kazi ya kujivua gamba na yeye na wenzake watajitahidi kuifanya kazi hiyo kwa haki bila kumwonea mtu.
Alisema alitangaza tangu Februari mwaka huu kuwa CCM itajivua gamba na sasa wameanza kuifanya kazi hiyo ingawa watu wengine wameanza kumtupia lawama Katibu wa Siasa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye aliyekuwepo katika tamasha hilo.
Kabla ya kutoa kauli hiyo katika Tamasha hilo la Pasaka, lililofanyika mjini Dar es Salaam, Askofu wa Kanisa la Assemblies of God Tanzania (TAG) Onesmo Ndegi, alisema hatua ya kujivua gamba inayochukuliwa na CCM chini ya Mwenyekiti wake, Rais Kikwete ina mkono wa Mungu.
Askofu Ndegi alisema sherehe za Pasaka mwaka huu ni maalumu kwa kuwa ni mwaka ambao Tanzania itaadhimisha miaka 50 tangu Uhuru ambayo katika Ukristo inaitwa Jubilee na maana yake ni kuweka kitu huru ama kukiondoa katika mateso.
Alisema kutokana na hali hiyo, Mungu amempa ujasiri Rais Kikwete wa kujivua gamba, kitendo ambacho CCM ilikianza hivi karibuni kwa kuwaondoa madarakani baadhi ya viongozi wake wa juu.
“Ujasiri wa Rais wetu ni ujasiri aliopewa na Mwenyezi Mungu pamoja na dua tunazomwombea, tunaomba kujivua gamba huko kuwe kwa ukweli na kusiishie hapo tu,” alisema Askofu Ndegi.
Baada ya kumaliza kusema hayo, Askofu huyo aliomba maaskofu wengine waliokuwepo ukumbini kumwekea mikono Rais sehemu waliko na kumwombea dua ya kumpa ulinzi, ujasiri na hekina katika uongozi wake.
Lakini Rais Kikwete pia alisisitiza umuhimu wa kudumisha amani nchini na kuwataka wananchi kuvumiliana baina ya watu wa dini mbalimbali na kutowasikiliza watu wanaohubiri habari za udini kwa lengo la kutaka kuleta mafarakano nchini.
Tamasha hilo ambalo Rais Kikwete alikuwa mgeni rasmi, lililenga kuchangisha fedha za kusaidia yatima, watu wenye ulemavu na mahitaji kwa wanawake wasiojiweza.
0 Comments